05 November 2010

Twiga Stars yale yale.

Na Mwandishi Wetu

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake, Twiga Stars jana ilifungwa mabao mawili 3-2 na Mali katika mchezo
uliopigwa Uwanja wa Sinaba, Afrika Kusini.

Kwa matokeo hayo, timu hiyo inakuwa imerudia mambo yale yale yanayofanywa na timu za Tanzania, ambazo zimekuwa zikifanya vibaya katika michuano mbali mbali ya kimataifa.

Hivi karibuni, Tanzania pia ilifanya vibaya katika michuano ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika nchini India, ambapo timu zake zilishindwa kuleta medali nchini na kurudi kama walivyokwenda.

Katika mechi ya jana, Mali ndiyo walianza kupata bao dakika ya 24, kupitia kwa Fortunata Diarra baada ya kupiga mpira kwa shuti la mbali lililomshinda kipa wa Twiga Stars, Fatuma Omary.

Kufungwa kwa bao hilo, kuliwazindua Twiga Stars ambao walipeleka mashambulizi ya nguvu na kusawazisha bao hilo dakika ya 29, lililofungwa na nahodha wake, Sofia Mwasikili ambaye alipiga mpira wa adhabu uliomshinda kipa wa Mali na kujaa wavuni.

Mali ilipata bao la pili dakika ya 31 lililofungwa tena na Fortunata, baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa kutoka wingi ya kulia ambayo mabeki wa Twiga, walishindwa kuondoa hatari hiyo.

Twiga Stars ilisawazisha bao hilo dakika ya 32, lililowekwa kimiani na Esther Chambruma.

Kipindi cha pili kwa timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini Mali ndiyo walipata bao la ushindi dakika ya 67 na Diaty N'diaye.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa inashika mkia katika msimamo wa kundi lake, ikiwa haina pointi linaloongozwa na Nigeria yenye pointi sita, ambayo itakutana nayo katika mechi ya mwisho.

No comments:

Post a Comment