03 November 2010

Vodacom yaitengea fedha Mitikisiko.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom, imetenga sh. milioni 22 kwa ajili ya Tamasha la Mtikisiko linalotarajia kufanyika katika mikoa ya Mbeya na Iringa.
Tamasha hilo linaandaliwa na Ibony Entertainment, litanza kurindima Novemba 6 jijini Mbeya ambalo litafanyika katika Uwanja wa Sokoine na lingine litafanyika Novemba 13, mwaka huu Iringa mjini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwakilishi wa tamasha hilo, Leah Mbeyale alisema tamasha hilo litashirikisha wasanii mbalimbali, wakiongozwa na bendi African Stars 'Twanga Pepeta'.

Alisema pia kutakuwapo na michezo mingine, ikiwamo pool table na masumbwi na burudani hizo lengo lake likiwa ni kufurahia burudani za tamasha hilo na kukutanisha vijana mbalimbali.

"Tangu lianzishwe tamasha hili, limekuwa na mguso mkubwa mkoani Iringa, kitu kilichotuongezea hamasa na hamu ya kuona mikoa mingine nayo inapata fursa ya kusherehekea tukio hilo, lenye dira na mguso kwa wadau wote wa Mbeya na Iringa.

"Wadau waje kwa wingi, kwani kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 5,000 huku ulinzi ukiwa wa kutosha wakati wote wa tamasha hilo ili mashabiki watakaofika waweze kujirusha vyema na midundo ya muziki," alisema Leah.

Naye Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga, alifurahia kudhamini tamasha hilo, huku akisema litakuwa maalumu kwa wadau wao, kuifahamu vyema Vodacom na kusherehekea pia miaka 10, tangu kuanzishwa kwake.

"Siku zote Vodacom inapenda kushirikiana na wadau wake katika mambo yote, huku wakiamini kwamba ndiyo fursa pekee ya kuwatumikia na kujitangaza kwao," alisema Leah.

Tamasha hilo pia litakuwa na burudani mbalimbali kutokana wasanii kochokocho wa kizazi kipya wanaotamba kwa sasa katika anga ya muziki huo.

No comments:

Post a Comment