03 November 2010

Simba yajificha Njombe.

Na Mwandishi Wetu

MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba wameweka kambi ya muda wilayani Njombe kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao, dhidi ya Majimaji ambapo leo watajipima
nguvu na timu ya Mji Njombe FC.

Timu hiyo iliwasili Dar es Salaam Jumamosi, ikitokea Mwanza walikoweka kambi, kuhudhuria msiba wa kocha wao wa viungo na mshauri wa benchi la ufundi, Syllersaid Mziray, aliyezikwa juzi katika makaburi ya Kinondoni.

Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Njombe Msemaji wa klabu hiyo, Cliford Ndimbo alisema wameamua kuweka kambi ya siku mbili, Njombe kabla ya kesho, kwenda Songea.

"Leo (jana) tunatarajia kucheza mechi yetu ya kirafiki na timu ya Mji Njombe FC, ili kocha aweze kukipima kikosi chake, kabla ya kuwavaa Majimaji hapo Jumapili," alisema Ndimbo.

Alisema waliamua kukatisha kambi na mchezo mmoja wa kirafiki, dhidi ya Mwanza United, kwa ajili ya kuhudhuria msiba wa Mziray na kwa kuwa ameshazikwa, waliamua kwenda Njombe kuweka kambi kabla ya kwenda Songea.

Ndimbo alisema wachezaji wake, wapo katika hali nzuri, isipokuwa Uhuru Selemani na Shija Mkina ambao walirudishwa Dar es Salaam kuendelea na matibabu.

Alisema wamejipanga kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo, ili wamalize mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni, kwani itawapa nguvu wachezaji wao katika mzunguko wa pili.

Simba ndiyo vinara wa ligi hiyo, baada ya kujikusanyia pointi 24 ikiwa pia tayari timu hiyo imepoteza michezo yake miwili na kushinda minane.

No comments:

Post a Comment