11 November 2010

Ruwa'ichi ateuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwanza.

Na Elisante Kitulo

BABA Mtakatifu Benedict XVI amemteua Mhashamu Askofu Jude Ruwa'ichi kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza.Askofu Ruwa'ichi, alikuwa Askofu wa
Jimbo la Dodoma, anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Askofu Mkuu,  wa Jimbo hilo, Antony Mayalla, aliyefariki dunia Agosti 19 mwaka jana.

Taarifa ya uteuzi huo imetolewa kupitia Balozi wa Papa nchini Askofu Mkuu Joseph Chennoth, na kusambazwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Akizungumza na Majira ofisini kwake Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Katibu wa TEC, Musinyori(msgr) Julian Kangalawe alisema uteuzi huo ulitangazwa duniani kote jana saa nane mchana.

Musinyori Kangalawe, alisema Askofu Ruwa'ichi alizaliwa Januari 30 mwaka 1954, Moshi mkoani Kilimanjaro na kupata daraja la upadri Novemba 25 mwaka 1981.

Aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paul wa II kuwa askofu Februari 9 mwaka 1999 na kupata daraja hilo Mei 18 mwaka huo.

Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma Januari 15 2005 nafasi ambayo amekuwa nayo hadi unapofanyika uteuzi huu.

Aidha, Askofu Ruwa'ichi,  ni Rais wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC) kwa wamu ya pili ya miaka sita.

Jimbo Kuu la Mwanza ni moja kati ya majimbo makuu matano ya Kanisa Katoliki nchini, mengine ni Dar es Salaam, Arusha, Tabora na Songea.

1 comment:

  1. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo amjalie Roho yake aweze kuhudumia vema ndugu zetu wa Mwanza, Kanisa na taifa lote la Tanzania. Katonji(DSM)

    ReplyDelete