02 November 2010

Ucheleweshaji matokeo wazua balaa.

Na Waandishi Wetu

UCHELEWESHAJI wa matokeo katika majimbo mbalimbali umezua balaa katika mikoa mitano nchini, hali iliyosababisha wafuasi wa vyama vya upinzani kuzingira ofisi za
wasimamizi wa uchaguzi na matokeo yake kutawanywa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Hali ya sintofahamu ilianza kujitokeza juzi usiku baada ya kuhesabu kura vituoni na mawakala kupata matokeo yao, hivyo mashabiki wa vyama vilivyojiona vimeshinda walikuwa na shauku ya kusikia matokeo rasmi bila mafanikio, hali ambayo ilianza kuhatarisha amani.

Baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na hali hiyo ni Jimbo la Ubungo, mkoani Dar es Salaa ambako taarifa za awali kutoka kwa mawakala zinasema kuwa Mgombea wa CHADEMA, Bw. John Mnyika ameibuka kidedea, Mwanza ambako mgombea wa Jimbo la Nyamagana pia kupitia CHADEMA, Ezehia wenje amemshinda Laurence Mmasha wa CCM na Arusha Mjini ambako ilithibitika jioni kuwa Bw. Godbless Lema kutoa chama hicho amembwaga Dkt. Batilda Burian wa CCM.

Maeneo Mengine ni Jimbo la Mbozi Magharibi ambako inadaiwa kuwa mgombea wa CCM, Bw. David Siyame ameshindwa na mgombea wa CHADEMA na mkoani Shinyanga ambako pia inadaiwa wagombea kadhaa wa CHADEMA walidaiwa kushinda.

Katika Wilaya ya Temeke, mashabiki wa Chama cha CUF, waliokuwa wanaandamana kupinga ushindi wa diwani wa CCM katika Kata ya Tandika walitawanywa kwa mabonu ya machoni na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Hali ilikuwa vivyo hivyo, katika Jimbo la Arusha mjini ambako umati wa wafuasi wa CHADEMA walijikusanya katika ofisi za Halmashauri wakitaka matokeo yatangazwe baada ya kutokea uvumi kuwa kuna mpango wa kubadili matokeo.

Hata hivyo, baada ya watu hao kukaa kwa muda, msimamisi alitangaza matokeo majira ya saa 12:00 jioni, hatua iliyosababisha wafuasi hao kuingia mitaani kushangilia.

Wakati wakishangilia, polisi walitumia maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na kurusha risasi za moto hewani kuwatawanya mashabiki hao.

Katika hatua nyingine, wilayani Mbozi mkoani Mbeya, mashabiki wa CHADEMA walioanza kusherehekea ushindi wa diwani mmoja wa chama hicho saa 9:00 usiku juzi, walianza kujongea kwenye eneo la kutangazia matokeo kusubiri kutangazwa kwa mbunge waliyeamini ameshinda kutoka chama chao, lakini hadi jana jioni matokeo hayakuwa yametangazwa.

Kutokana na hali hiyo, mashabiki hao walianza kushinikiza kutangazwa kwa matokeo, ndipo FFU walitokea wakiwa rasmi na kuanza kuwatawaya kwa mabomu, ambapo kijana Jonas Shonda alijeruhiwa kichwani.

Halikadhalika mjini Shinyanga na jijini Mwanza FFU walilazimika kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakishinikiza matokeo yatangazwe haraka, ambayo waliamini kuwa yanacheleweshwa ili kuyachakachua baada ya wagombea wa CCM kushindwa.

Katika vurugu hizo, ofisi ya CCM Kata ya Isamilo ilichomwa moto, gari la Kamanda wa Polisi mkoa wa mwanza lilivunjwa vioo na gari la kiongozi mmoja wa CHADEMA ambaye jina halikupatikana pia lilichomwa moto. Hatimaye Msimamisi alitangaza kushindwa kwa Bw. Masha.

Vile vile wakati tunakwenda mitambini zilipatikana taarifa kuwa wafuasi wa CHADEMA katika Jimbo la Kawe walikuwa wanaandamana kudai kutangazwa kwa matokeo, wakiwa wanaamini kuwa mgombea wao, Halikma Mdee alikuwa ameshinda.

Imeandaliwa na David Magesa, Glory Mhiliwa, Rashid Mkwinda, Rabia Bakari.

No comments:

Post a Comment