02 November 2010

CHADEMA wapiga wasimamizi, CCM wachoma nyumba.

Na Faida Muyomba, Geita

NYUMBA nane pamoja na maduka mawili katika kitongoji cha Makanda, Kata ya Nyamalimbe zimeteketezwa kwa moto na wasimamizi wawili
wasaidizi Kata ya Nyakagomba wamejeruhiwa vibaya katika matukio tofauti jimboni Busanda.

Katika tukio la kwanza la Nyakagomba, tarafa ya Butundwe lililotokea saa mbili usiku jana, wasimamizi wawili wa kituo cha Shule ya Sekondari Butundwe na Bw. Uwezo Kalikona (26) na Bw. Frank Mugeta (26) walijeruhiwa vibaya na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA.

Wasimamizi hao walipigwa na wafuasi hao baada ya wakala wa chama hicho kubaini kuwa wagombea wao walikuwa wameshinda katika kituo hicho, ambapo alitoka nje ya kituo mbio
na kupiga mayowe kuashiria ushindi wakati matokeo bado hayajabandikwa.

Akisimulia tukio hilo akiwa wodini hospitali ya Wilaya ya Geita, mmoja wa majeruhi hao, Bw. Kalikona alisema, "wakala huyo baada ya kuona kuwa wameshinda, alimuomba ruhusu mgambo na kumwambia kuwa anasikia tumbo linamvuruga na ndipo alitoka nje badala ya kwenda kujisaidia alianza kupiga mayowe ambapo wafuasi wa chadema waliokuwa wamejificha walifika na kuanza kurusha mawe dirishani wakitaka tutangaze
matokeo."

Aliendelea kuwa, "Tuliwaomba muda wa kuandika matokeo hayo katika karatasi maalumu na walituruhusu huku wakiwa wanatupiga kwa mawe na baadaye tuliwapa, waliposoma
walituamuru kuyabandika na tukatekeleza lakini baadaye walidai kuwa wakala wao yuko wapi, wamepata taarifa kuwa tumemuua."

Baadaye wafuasi hao wanadaiwa walizidi kuwapiga kisha kuwapekua mifukoni ambapo hawakujua kilichoendela tena, kwa kuwa walipoteza fahamu kwa muda na kujikuta hospitali ya
wilaya ya Geita huku wote wakiwa na majeruhi katika sehemu mbalimbali za mwili.
 
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dkt. Omar Dihega alikiri kuwepo kwa majeruhi hao na kwamba hakuna aliyefariki dunia
kama ilivyokuwa imedaiwa hapo awali.

Alisema majeruhi wote walipata majeraha sehemu za kichwani, mikononi na sikioni ambapo mmoja wao, Bw. Mugeta alipigwa picha ya X-RAY na wote kwa sasa wanaendelea vizuri.

Katika tukio jingine nyumba nane na maduka mawili ambayo yanasadikika kuwa na ya wafuasi wa CHADEMA zimechomwa moto na kuteketea na wafuasi wa CCM.

Tukio hilo lilitokea jana saa tano usiku, katika Kitongoji cha Makanda baada ya kuwepo na fununu kuwa CHADEMA imeshinda udiwani katika eneo hilo.

Habari zilizo patikana kutoka eneo la tukio hilo, zilidai kuwa vurugu hizo zilianzishwa baada ya matokeo ya awali kucheleweshwa kutangazwa ambapo wafuasi CHADEMA kuvamia kituo wakitaka kuyachoma masanduku ya kura.

Hata hivyo wasimamizi wa kituo hicho walifanikiwa kubandika matokeo hayo na kukimbia baada ya kuona fujo zinaongezaka ambapo wafuasi wa CCM kutoka katika kitongoji jirani cha Bubede kupata taarifa kuwa katika kitongoji cha Makanda CHADEMA iliongoza kura za udiwani.

Chanzo chetu cha habari kiliendelea kueleza kuwa wafuasi hao wa CCM baada ya kuona matokeo walianza kuchoma nyumba hizo wanazozijua kuwa ni za wafuasi wa CHADEMA na kuvunja ofisi ya chama hicho.

Kamanda wa polisi Mkoani Mwanza, Bw. Simon Sirro, katika mazungumzo ya simu na Majira alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na
jeshi hilo.

No comments:

Post a Comment