Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeitaka timu ya taifa ya wanawake 'Taifa Stars' kukaza buti kwa kujipanga upya katika fainali za saba za
Mataifa ya Afrika za wanawake zinazoendelea nchini Afrika Kusini.
Twiga Stars ilianza mashindano hayo kwa kufungwa mabao 2-1 na wenyeji Afrika Kusini 'Banyana Banyana' katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sinaba nchini humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, alisema walianza vibaya mashindano hayo kwa kufungwa, lakini Twiga Stars haina budi kushinda katika michezo inayofuata.
"Novemba 4 (kesho) Twiga Stars, itacheza na Mali na kumalizia na Nigeria Jumamosi, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanashinda katika michezo hiyo, ili isonge mbele na hatimaye itwae ubingwa," alisema Kayuni.
Alisema anawaomba Watanzania waliopo nje ya nchi na wa ndani kuiombea timu hiyo ifanye vizuri, pamoja na kuwatia moyo kuhakikisha inaitoa kimasomaso nchi katika mashindano makubwa kama hayo.
Twiga Stars ipo kundi A na timu za Nigeria, Mali na wenyeji Banyana Banyana ambapo Nigeria ndiyo inayoongoza kundi hilo kwa pointi tatu, ikiwiana na Banyana Banyana ila zinatofautina kwa mabao ya kufunga ambapo, Nigeria ina matano baada ya kuifunga Mali na wenyeji ina mawili.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), mashindano hayo yalitarajiwa kuendelea jana kwa kupigwa michezo miwili ya Kundi B ambapo, Equatorial Guinea iliumana na Cameroon na Algeria dhidi ya Ghana.
No comments:
Post a Comment