*Yataka wachezaji bora Ligi Kuu
Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limezitaka klabu mbalimbali zinazoshiriki mashindano yao, hususan Ligi Kuu Bara kusajili wachezaji
watakaowasaidia na si bora wachezaji.
Usajili wa dirisha dogo ulifunguliwa rasmi Novemba Mosi, mwaka huu duniani kote ambapo kwa hapa nchini klabu zinazoshiriki mashindano ya TFF, kuanzia ya Ligi Daraja la Tatu mpaka Ligi Kuu, shughuli hiyo imekwenda kwa pamoja.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, alisema huu ni wakati muafaka kwa kila klabu kurekebisha vikosi vyao, ili kufanya ligi ziwe za ushindano.
"Unajua kipindi hiki cha usajili cha dirisha dogo ni cha Dunia nzima ambapo kitakwenda mpaka Novemba 30, hivyo ni wajibu wa klabu kusajili wachezaji watakaozisaidia timu zao ni kusajili tu," alisema Kayuni.
Alisema anavikumbusha vyama vya Wilaya na Mikoa, kuhakikisha vinasimamia shughuli hii kwa ufasaha na kuhakikisha wanafuata taratibu husika, pamoja na ukomo wa kufanya usajili.
Wakati huo huo, Kayuni aliongeza kwamba waamuzi watatu ambao wanaendelea na uchunguzi na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), watawapanga katika kucheza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Aliwataja waamuzi hao ni Oden Mbaga, Hamis Chang'walu na Jesse Erasmo ambao baada ya FIFA, kugundua wana matatizo (bila kuyajata) waliamua kuwasimamisha, ili wafanye uchunguzi lakini wakiwa wanasubiri ripoti kutoka huko wakashangaa kuona wakiwaruhusu kuchezesha mchezo mmoja huko Botswana.
"Unajua hili suala linaonekana lina utata, hivyo kama wao (FIFA) waliwatumia katika mchezo wa U-23 kati ya Botswana na Namibia, sasa na sisi tunaona ni bora tukawatumia katika michezo ya Ligi Kuu, kuliko kuwaacha tu kwani tunahofia viwango vyao kushuka," alisema Kayuni.
No comments:
Post a Comment