03 November 2010

Makocha wamiminika Azam FC.

Na Addolph Bruno

SIKU moja baada ya kukatisha mkataba na kocha wao Itamar Amorin, uongozi wa Klabu ya Azam FC umesema umeanza kupokea maombi ya makocha
kuinoa timu yao kutoka katika nchi za Denmark, Sweden, Burgalia na Serbia.

Azam ilitangaza kusitisha mkataba na Amorin juzi, ambaye mkataba wake ulitakiwa kufikia kikomo Aprili, mwakani kutokana na kilichodaiwa kuwa wameamua kufanya hivyo kwa maslahi ya kocha huyo, klabu na wachezaji.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrisa Nassor alisema makocha hao wametumia njia mbalimbali kufikisha maombi yao kwa uongozi wa klabu hiyo na kwamba bado wapo katika mchakato mzito wa kuhakikisha wanapata kocha atakayekidhi viwango.

"Na hii ni kusema kwamba tunawakaribisha na wengine milango ipo wazi, kama mtu anaona ana sifa zote na uzoefu wa kutosha katika kufundisha mpira wa miguu tunamkaribisha," alisema Nassor.

Alisema wanaendelea kupokea maombi na kwamba mpaka mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, utakapoanza watakuwa na kocha mwingine wa kuziba pengo la Amorin, ambapo kwa sasa timu yao ipo chini ya kocha msaidizi Habibu Kondo.

Katibu huyo alisema wachezaji wamelipokea vizuri suala hilo na amewataka kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki, wakifikiria zaidi kuipatia ushindi timu yao.

Hata hivyo Nassor, alisisitiza kuwa wamekatisha mkataba na kocha huyo kwa amani na hakuna sababu nyingine ya msingi, ambayo imesababisha kuvunja naye huku akipinga madai yaliyowahi kutolewa kuhusu kumchukua kocha Patrick Phiri wa Simba.

"Wengine wamekuwa wakitoa taarifa zisizo rasmi kuwa tunamhitaji, Phiri lakini suala hilo halipo kwa sababu yule tayari ana mkataba na Simba huo ni uzushi hakuna ukweli hata kidogo," alisema Nassoro.

Katika hatua nyingine, Nassor alisema timu yake imeondoka jana kwenda Tanga tayari kumenyana na Ruvu Shooting, katika mchezo wa mwisho mzunguko wa kwanza utakaochezwa Jumapili Uwamja wa Mkwakwani, Tanga.

No comments:

Post a Comment