05 November 2010

Simba kujenga uwanja wa Kisasa.

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba inakaribia kujenga Uwanja wa kisasa, utakaochukua miezi 24 katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam utakaochukua watu 30,000.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Aden Rage alisema katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokutana juzi, kilipitisha kwa kauli moja azimio hilo.

Alisema uwanja huo utakamilika baada ya miezi 24, ambapo Kampuni ya GIDAS ya Uturuki ndiyo iliyopewa tenda na kati ya Novemba 15 mpaka 25, mwaka huu, watapokea ujumbe wa watu kutoka kampuni hiyo, watakaofanya upembuzi wa awali na makubaliano ya msingi na klabu.

"Kama mnavyojua tuna eneo kubwa kule Bunju, hivyo kwa kauli moja tumeazimia kujenga uwanja wa kisasa ambao utakuwa na maduka ya biashara, yatakayokodishwa kwa wafanyabiashara mbalimbali," alisema Rage.

Alisema pia Chuo Kikuu Huria Tanzania(OUT), kimeahidi kutoa wataalamu wao watakaoungana na wale wa GIDAS, kuhakikisha uwanja huo unajengwa katika kiwango kinachohitajika.

Mbali na hilo, Rage alisema katika kikao hicho pia walikubaliana kuunda Kamati ya Ufundi, itakayongozwa na Ibrahim Masoud 'Maestro', akisaidiana na Abdallah Kibaden 'King', Said Tuli, Khalid Abeid, Daniel Manembe na Avodius Mtawala ambaye atakuwa Katibu wa kamati hiyo.

Akizungumzia suala la Kocha Mkuu, Patrick Phiri kuhusu hatma yake ya kuifundisha timu hiyo, alisema Kamati ya Utendaji imemwongezea mkataba (bila kutaja wa muda gani) na kumpandisha cheo, ambapo licha ya kuwa Kocha Mkuu pia atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.

Alisema pia imemteua Kibadeni kuwa Kocha Mkuu wa timu zao za vijana chini ya umri wa miaka 14 na 17 ambapo wana imani kutokana na uwezo aliokuwa nao na uzoefu, timu hizo zitakuwa na wachezaji wazuri.

2 comments:

  1. Hongera uongozi wa Simba kwa kuwa na program zuri kwa ajili ya maendeleo ya klabu.

    ReplyDelete
  2. Hongera Simba kwa mipango mizuri mliyokuwa nayo, tunaomba mipango hiyo isiishie kwenye makaratasi tu.

    ReplyDelete