08 November 2010

Meya, naibu wake waangushwa Shinyanga.

Na Suleiman Abeid, Shinyanga
 
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini kimepata pigo baada ya wagombea wake sita katika viti vya udiwani akiwemo aliyekuwa Meya na
Naibu wake kuangushwa na wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
Katika uchaguzi uliomalizika wiki iliyopita wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM katika kata za Kambarage, Kitangili, Ibadakuli, Ngokolo, Ndala na Masekelo
waliangushwa vibaya na wagombea wa CHADEMA ambapo kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe hapa nchini Manispaa ya Shinyanga itakuwa na madiwani kutoka
vyama vya upinzani.

Hata hivyo, chama hicho kimeendelea kuongoza halmashauri ya manispaa ya Shinyanga baada ya kujipatia madiwani 11 dhidi ya sita wa CHADEMA.
 
Katika Kata ya Kambarage aliyekuwa Meya wa Manispaa kwa tiketi ya CCM, Bw. Hassan Mwendapole aliangushwa na mgombea wa CHADEMA, Bw. Nyangaki Shilungushela na
aliyekuwa Naibu Meya katika Manispaa hiyo, Bi. Moshi Kanji alishindwa na mgombea wa CHADEMA, Bw. George Kitalama.
 
Wilayani Meatu katika kata ya Bukundi aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM katika kipindi kilichopita, Bw. Joseph Masibuka amefanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa mara nyingine kwa kupitia CHADEMA.

Bw. Masibuka alijiengua ndani ya CCM mara baada ya jina lake kukatwa katika kura za maoni ndani ya chama hicho, na badala yake kuteuliwa aliyekuwa mshindi wa tatu.
 
Bw. Masibuka ameahidi kutekeleza ahadi zake kwa wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote wala kinyongo kwa viongozi wake wa zamani wa CCM.

3 comments:

  1. Viongozi wa nchi hii inabidi mmurudie Mwenyezi Mungu.Kweli katika kinyang'anyiro cha ubunge inakuwaje mtu kama Chenge anapitishwa,ana kashifa ya rushwa,dharau pia ana kesi ya kuua.Mtu huyu hastahili hata ubalozi katika nchi za watu wenye mwono mpana kama Kenya,Rwanda na Nigeria.Nchi hii inamfaa Kagame kwa marekebisho,labda tumwombe atusaidie kwa mwaka mmoja.Ebu angalia mtuhumiwa wa rushwa katika nchi hizo au mbadirifu wa pesa za umma anavyofanywa.Mali yake yote hutaifishwa na anabaki na adabu.Ionee huruma Tanzania na watu wake.

    ReplyDelete
  2. inauma sana, dharau za chenge anatufanya watanzania wote hatuna akiri

    ReplyDelete
  3. Chenge huyu hafai katika jamii,tena anatia aibu chama chake na vile vile anaaibisha nchi yetu kwa ujumla.Kwanza ni mbinafsi,ana tamaa na pia ni muongo.Hakubali kabisa kuwa yeye ni fisadi,kwanini?Uspika anautafutia nini?hafai huyu hata huo ubunge kaupata kwa njia isiyo halali.

    ReplyDelete