KAMPALA,Uganda
KIONGOZI wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC),Dkt. Kizza Besigye amezindua kampeni zake za kuwania kiti cha urais katika Wilaya ya Masaka
huku akitoa ujumbe wenye matumaini kwa raia wa nchi hiyo.
Habari kutoka nchini humo zilieleza jana kuwa Dkt.Besigye alizindua kampeni zake juzi na kuwataka wananchi kutokata tamaa katika kutafuta utawala bora.
"Kuweni na nguvu na nia ya kuchagua hatima bora. Kama mtachukua uamuzi thabiti kwa kupiga kura katika uchaguzi huu itatokea na tutafanikiwa hivi karibuni, "Besigye alisema kwa kutumia lugha ya Kiganda.
"Bunduki haiwezi kushinda nguvu ya umma. Rais Museveni yeye anajua ni bora kwa sababu alikwenda mstuni na bunduki 27 na kushinda serikali ya Obote kwa jeshi, bunduki nyingi na fedha, "alifafanua.
Dkt.Besigye, ambaye ni mgombea kupitia muungano wa vyama alisema kuwa umaskini,ukosefu wa dawa kwenye vituo vya afya,elimu duni,kodi kubwa,ukosefu wa ajira,kutoheshimu viongozi wa jadi kama Kabaka,rushwa na ukabila vinaweza kutatuliwa kwa kufanya mabadiliko.
“Rais anapaswa kuwa mtumishi wa watu,lakini Museveni anapokuja hapa mnampigia makofi huku mkimueleza aendelee kuwa rais jambo ambalo linamfanya ajifikiri kuwa ni bosi, abaki ili afanye nini?,hivyo basi umaskini na ujinga ni lazima vitaendelea,"alisema Dkt. Besigye.
“Fedha zinakusawanywa kutoka kwa raia wengi wa Uganda lakini zinawanufaisha wachache;ndugu, marafiki na wajomba huku wauza maduka wakishinda wanapambana na nzi kwa sababu hakuna wanunuzi wa bidhaa zao,watu ni maskini na vijana hawana ajira,"alifafanua katika mkutano huo wa kampeni.
Dkt. Besigye aligeukia pia upande wa kilimo ambapo alisema kuwa mkulima amekuwa hanufaiki ipasavyo na kilimo kama matumizi yake yalivyo na akatolea mfano katika Wilaya za Bunyoro na Kiboga ambapo kilo moja ya mahindi inauzwa sh.100.
“Unauza gunia la mahindi kwa Sh.10,000 na unakwenda dukani unanunua kilo tatu za sukari,”alisema na kuibua kicheko kwa wafuasi wake.
Dkt Besigye alisema kuwa pindi atakapochukua madaraka ataanzisha utaratibu wa Serikali shirikishi.
Kiongozi huyo aliwasili katika eneo la Lukaya saa 3 asubuhi ambapo na kutambulishwa kwa wananchi na Katikkiro wa zamani wa Buganda, Bw.Joseph Mulwanyammuli Ssemwogerere,na kisha kuanza safari ndefu ya kuzungukia vijiji vya Lwabenge na Bigasa na kuwahutubia wananchi kial mahali aliposimama kabla ya kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika eneo la Bukomansimbi.
Iliripotiwa kuwa baada ya mkutano huo Dkt.Besigye alielekea katika maeneo ya Butenga, Buyoga, Misanvu, Kyabakuza, Kyakumpi na Nyendo kabla ya kuhutubia mkutano huo mkubwa katika kituo cha watoto kilichopo katika Manispaa ya Masaka.
No comments:
Post a Comment