04 November 2010

Spurs yaitolea uvivu Inter Milan.

LONDON, England

TIMU ya Tottenham Hotspur ya England, usiku wa kuamkia jana iliwachapa mabingwa watetezi wa michuano ya Kalbu Bingwa Ulaya, Inter Milan
mabao 3-1, katika mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa White Hart Lane, England.

Timu hizo za Kundi A, zilikuwa zikicheza mechi ya pili, katika mechi ya kwanza Inter Milan iliifunga Tottenham mabao 4-3, kwenye Uwanja wa San Siro mjini Milan.

Mchezaji Rafael Van der Vaart, alikuwa wa kwanza kuifungia Tottenham bao dakika ya 18, kabla ya kutolewa nje kwa maumivu.

Mshambuliaji wa pembeni wa Tottenham, Gareth Bale, alitoa mchango mkubwa wa bao la pili lililofungwa na Peter Crouch dakika ya 61, kabla ya Roman Pavlyuchenko kumalizia bao la tatu dakika ya 89.

Mshambuliaji nyota wa Inter, Mcameroon, Samuel Eto'o aliifungia bao dakika ya 80.

Nayo Manchester United, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bursaspor, iliyopigwa nchini Uturuki na kukaribia kucheza robo fainali ya michuano hiyo.

Darren Fletcher alikuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za wapinzani wao wa Kundi C, dakika ya 48, kabla ya Gabriel Obertan kuongeza bao la pili dakika ya 73 na Tiago Bebe kumalizia bao la tatu dakika 77.

Kundi D, vinara Barcelona, iliminywa na FC Copenhagen na kutoka sare ya bao 1-1, kwenye Uwanja wa Parken.

Barca walikuwa ushindi nchini Denmark, ungewawezesha kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo, bao lao lilifungwa dakika ya 31 na Lionel Messi.

FC Copenhagen ambao wako nafasi ya pili ya kundi lao, ilisawazisha bao hilo haraka kupitia kwa Claudemir.

Lyon ilichapwa mabao 4-3, dhidi ya Benfica, mechi ya Kundi B.

Nayo FC Twente ilirejesha matumiani ya kucheza robo fainali, baada ya kuibamiza Werder Bremen mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment