04 November 2010

Slaa aitaka NEC isitishe matokeo.

*Adai yanayotangazwa ni tofauti na kura za vituoni.
*Asema yameandaliwa makusudi kumbeba mgombea wa CCM.
*NEC yasema kama ana ushahidi awasilishe vielelezo.


Na Tumaini Makene
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa amesema zimefanyika njama kuhujumu matokeo ya uchaguzi mkuu
hasa katika nafasi ya urais ili kumbeba mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama chake, Rais Jakaya Kikwete.

Kutokana na hali hiyo ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha mara moja utangazaji wa matokeo unaoendelea kwa kuwa yanatofautiana na idadi halisi ya kura zilizohesabiwa vituoni, kisha irudie uchaguzi wote katika nafasi ya urais.

Dkt. Slaa aliongeza kuwa chama chake kina ushahidi, na mwingine kinaendeleea kuufanyia kazi, unaoonesha namna ambavyo matokeo yanayotangazwa na NEC ni tofauti na yale yaliyopatikana vituoni baada ya upigaji kura.

Mbali ya nafasi ya urais, mgombea urais huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema kuwa uchaguzi unapaswa kurudiwa katika nafasi ya ubunge katika majimbo ambako matokeo yake yameonekana kuwa na utata mkubwa, akitolea mfano wa Jimbo la Segerea na maeneo mengine nchini.

Dkt. Slaa aliyasema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alisisitiza kauli yake ya mara kwa mara kuwa hawezi kuzungumza bila kuwa na ushahidi au kufanya utafiti, akionesha namna ambavyo chama chake kimefanyiwa kile alichodai kuwa ni hujuma, kutokana na kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi.

"Tumeamua kuzungumzia mwenendo wa mambo haya sasa kwa sababu tunajua tofauti na udiwani au ubunge ambapo unaweza ku-challenge (kupinga) ushindi mahakamani, urais huwezi, hata kama matokeo yatakuwa na dosari, huwezi kwenda mahakamani wala kuhoji popote, hivyo lazima tuseme sasa...tunapenda kutoa tahadhari kwa vyombo vya ulinzi na usalama na NEC yenyewe kuna mambo yametushtua sana, taratibu zimekiukwa sana.

"Kwanza walianza kisaikolojia, mnakumbuka gazeti la serikali lilisema Slaa hawezi kuwa rais, akaja mnadhimu mkuu wa jeshi naye akasema yake, mkuu wa polisi naye hivyo hivyo, wakisisitiza tukubali matokeo, wanasaikolojia tukawa tunajiuliza ni kitu gani kinaandaliwa, sisi tulisema mapema matokeo tutayakubali iwapo mchezo ukifuata taratibu," alisema Dkt. Slaa na kuongeza.

"Nitazungumzia zaidi upande wa urais, tangu matokeo yaanze kutolewa kulikuwa na mkakati maalumu, NEC ikawa haitangazi matokeo ya maeneo yale ambayo tuna nguvu, si kitu kidogo hicho, walianza Zanzibar yakamalizika majimbo yote, wakaja maeneo mengine ya bara...ilikuwa inajengwa dhana kisaikolojia kuwa CHADEMA iko huko mwishoni na ni ya kushindwa tu, sisi tukaanza kukusanya data huko chini kukoje."

Huku akitoa mifano ya baadhi ya vituo katika majimbo kama vile Same Mashariki, Mheza, Segerea, Hai, Kiteto, Kibakwe, Kyela, Morogoro Mjini na mahali pengine, Dkt. Slaa alisema kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi, ili kutimiza kile alichodai ni 'kucheza na namba za matokeo na saikolojia za watu', kazi ambayo, inaonekana imefanywa kitaalamu na watu makini.

Akitumia maeneo hayo kama sampuli ya nchi nzima, Dkt. Slaa alidai kuna mahali kura zimepinduliwa kwa ama kuongezwa au kupunguzwa kwa pande zote mbili za CCM na CHADEMA, kukosekana kwa fomu za matokeo, kuwepo kwa vituo bandia vya kupigia kura, kutangazwa kwa matokeo ya urais na ubunge bila kuwa yamejumlishwa, wala masanduku ya kura kuwepo eneo la kujumlishia.

Alitaja baadhi ya mambo aliyoita hujuma, kuwa ni kutokuonekana kwa matokeo ya baadhi ya vituo mpaka wakati wa hesabu za mwisho na matokeo kutangazwa, (mathalani Kata ya Kiwalani, Tabata na Vingunguti huko Segerea). Pia wasimamizi wa vituo kuondoka na fomu za matokeo badala ya kukusanywa mbele ya mawakala, kutoshirikisha mawakala wakati wa kujumlisha.

"Sasa tunataka kuwauliza NEC kama maeneo mengine fomu hazikuwepo, au masanduku yalikuwa hayajafika eneo la kujumlishia wilayani, wamepata wapi hesabu za kutangaza matokeo ya kitaifa? Wanacheza na matokeo na saikolojia za watu...kwa mfano huko Same katika moja ya vituo, Kikwete alipata kura 92, Slaa alipata kura 69, lakini wao wakatangaza Kikwete 123 na Slaa 33.

"Wakaweka kituo hewa, wakacheza na namba, katika kituo halali, Kikwete akapata kura 190, Slaa kura 26, lakini zikazidishwa mara mbili zionekane ni za kituo kimoja, huko Mheza CCM walipata 92, CHADEMA 57 na CUF 71, lakini walipotangaza wakasema CCM 359, CHADEMA, 15 na CUF 23.

"Huko Geita matokeo halisi katika kata 20 yanaonesha kuwa CCM walipata 30,960, CHADEMA kura 15,736 lakini ilivyotangazwa na NEC taarifa zikakinzana, wakazipunguza na kuweka CCM 17,792, CHADEMA 3,789...hii maana yake nini, unacheza na namba kwa sababu zile za mwanzo ukisema Dkt. Slaa ana kura elfu kumi na tano ataonekana ni tishio lakini ukisema anazo elfu tatu, unamwonesha kuwa ni mtu wa kushindwa. 

"Sina neno jingine la kuita kitendo hiki, bali huu ni wizi mkubwa. Matokeo yanayotangazwa na NEC si yale yaliyopatikana vituoni, tunapigiwa simu na watu wetu wakishangaa hiki ni kitu gani, mahali pengine matokeo yametangazwa bila kuwepo kwa fomu za uchaguzi au za matokeo, mahali pengine watu wetu hawajashirikishwa katika zoezi la kuhesabu au kujumlisha kura, kisha wanaambiwa kuwa mambo yamekamilika.

"Hatujalala tunafanyia kazi mambo haya ili hasa tujue maana yake, ninao uzoefu wa wizi wa kura  unaofanywa na CCM huko Karatu...tumeagiza ushahidi zaidi uletwe kutoka huko vituoni, mwingine bado tunaofanyia kazi...tunashangazwa hata na asilimia za waliopiga kura, zingine zinafika hata asilimia elfu mbili au zaidi.

"Baada ya kuona mwelekeo huo, ninaomba NEC, tena natumia polite language (lugha ya upole), naiomba NEC...kama kweli tunaitakia mema nchi hii, kama kweli tuna utashi mwema na nchi hii, NEC ifute matokeo yote ya urais na kura zirudiwe upya...hatuwezi kukubali matokeo yaliyopikwa na usalama wa taifa, matokeo haya si ya kura za wananchi," alisema Dkt. Slaa na kuongeza;

"Tunataka mkuu wa usalama wa taifa ajiuzulu, hatukumuajiri awe usalama wa chama kimoja, jumuiya ya kimataifa waweke taarifa zao hadharani kama walivyoanza leo katika vyombo vya habari, taasisi za serikali kama TEMCO, nasikia hawa wamezuiwa kutoa matokeo yao ya uangalizi, tunataka zitoe taarifa zao, wasaidie nchi, si Kikwete wala CCM."

Dkt. Slaa alisema kuwa dosari nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita, kwa kiasi kikubwa zimetokana na maelekezo, akitolea mfano wa barua mbili zilizokamatwa hivi karibuni huko Mwanza, zikielekeza kuondolewa kwa majina ya vijana ili wasipigie upinzani, kuchelewesha utoaji matokeo, kutumia vijana wa green guards, matumizi ya nguvu ya polisi kutisha watu.

"Watanzania wakiishiwa uzalendo na uvumilivu kisha kuamua kuingia mitaani kama tulivyoona huko Geita, Shinyanga, Mwanza na kwingineko nani atakayebaki au kulaumiwa? Kikwete alisema vurugu zikianza wapinzani watapanda ndege kuondoka nchini, kumbe alijua anataka kufanya uchakachuaji huu waliofanya," alisema Dkt. Slaa. 

20 comments:

  1. Frankly speaking, hujuma iliyofanyika ni kubwa mno. Kwa nini watu wa usalama wanatufanyia hivi, kwa nini tuongozwe kibepari? Dr tuko pamoja kwa huu wizi uliofanywa na chama tawala.

    ReplyDelete
  2. ni aibu kubwa sana tunadhalilishwa na CCM.

    ReplyDelete
  3. hakika utashi wa uweli na uwazi unahitajika,tanzania ya leo sio ile ya mwaka wa 47,wakati ule tulikuwa tumnapelekwa kibepari,now we are educated we need really uongozi na sio bora uongozi wa kibabe nec nawatakia kazi njema

    ReplyDelete
  4. CCM ni majizi yanayojali masilahi yao tu bila kuona adha wapatayo wananchi hasa wakipato cha chini. Viongozi wa vyombo vya usalama wanaogopa kupoteza nyadhifa zao CCM ikianguka hivyo kwa namna yoyote ile wanahakikisha wanaibakisha CCM madarakani. Kuleni lakini kumbukeni pia kuna kufa

    ReplyDelete
  5. hata kama ni wizi mkubwa lakini bado dokta slaa hukua na uwezo wa kumshinda kikwete la maana hapa ni kijipanga vizuri kwa ajili ya mwaka 2015 unaweza kushinda iache tanzania iwe na amani

    ReplyDelete
  6. Kama ni hivyo machungu ya watanzania wapenda maendeleo hawata vumilia lakini wakumbuke kwamba huwezi kubadilisha mawazo ya watanzania kwa kutumia vitisho tukumbuke kuwa Mfalme Belshaza alianguka kwa aibu, huu mbuyu utadondoka tuu,ndipo watu watakapo aibika hadhrani

    ReplyDelete
  7. Kwa style hii ya uchakachuaji lazima Tanzania tutamwaga damu na kuwafuata wasomali,kenya na sudan.CCM na Usalama wa Taifa aka usalama wa CCM wamekusudia kuwanyang'anya watanznia amani yao na kuwaletea fujo,vita na mauaji.MTAJIBU HILI .....SIKU ZINAHESABIKA AMANI YA TANZANIA KUPOTEA,TUJIANDAE KUWA WAKIMBIZI

    ReplyDelete
  8. SLAA ACHA KUCHONGANISHA WANANCHI NA SERIKALI WEWE NDIYE UNAYEANZISHA WAZO LA KUFANYA FUJO SI WATANZANIA, JIPANGE KWA WAKATI MWINGINE HASA ANGALIA KUPATA WANACHAMA ZANZIBAR KWANI HUWEZI KUPATA KURA ZA BARA PEKEE NA UKAPATA USHINDI ZENJI BADO HUNA KURA!! KULALAMIKA PEKE SIO DAWA

    ReplyDelete
  9. DR, SILAHA WACHA RONGORONGO ZAKO MAANA UMETIA CHUMVI MCHUZI MPK UMEUHARIBU UMEANZA KULALAMIKA MNO KUANZIA KAMPENI MPK LEO, WEWE NI LAWAMA AU NDIO MBINU ZAKO ZA KUTAKA KUANZISHA FUJO?FURAHIA UMEWEZA KUJINYAKULIA VITI ZAIDI TOKA 6 MPK 24, LEO WEWE KILA KITU UNAKIJUWA SANA,KULIKO WENZAKO ILIKUWAJE UKAWAWEKA MAWAKALA AMBAO SI WAAMINIFU AU WEWE KILA SIKU UNADAI NUSU YA USALAMA WA TAIFA WANARIPOTI KWAKO IWEJE WAMESHINDWA KUDHIBITI HILO? WACHA KULALAMA JIPANGE KWA YAJAYO CHUNGUZA UPYA WAPI ULIPOJIKWAA SIO UANGALIE ULIPOANGUKIA = KIGMB

    ReplyDelete
  10. MKUKI KWA NGURUWE WE ULVYO MWIBA MKE WA MTU UNAFIKIRI HAIUMI,KESI INAKUNGOJA MAHAKAMANI WAKUMALIZE KISIASA,WEWE WALA CAHAMA CHAKO HAMNA UWEZO WA KUINDOA CCM JENGENI DEMOKRASI NDANI YA CHAMA CHENU KWANZA KUONDOA UBINAFSI BADO TUKUMBUKA YA WANGWE,KAFULILA VITI MAALUMU YOTE HAYO YAMECHANGIA KUANGUKA KWAKO,KIBAYA ZAIDI UBUNGE PIA UMEUKOSA JAMBO AMBALO TULIKUSII UBAKI KUWA MBUNGE MATOKEO YAKE NDIO HAYO UMEACHA MKEO KWA MKE WA MTU NA UNAKESI YA KUJIBU WE WAZAA.

    ReplyDelete
  11. Dr Slaa hilo liko wazi kuwa umeibiwa kura, lakini fikilia njia nzuri ya kufuatilia haki yako, Tuko pamoja. Hawa wanaotoa maoni ya ajabu juu yako kisaikolojia bado pia wanaonesha kuwa ulikuwa juu na ndio maana lugha zao c nzuri, PENYE JIPU PANALINDWA PASIUMIZWE MPAKA PAIVE.

    ReplyDelete
  12. JAMBO LA KUMWIBA MKE,SIYO HOJA,HOJA NI KWAMBA JE KURA ZIMEIBWA??NA KAMA ZIMEIBWA NJIA ANAYOTUMIA DR SLAA NI SAHIHI?? ILI NI JAMBO LA KISHERIA ZAIDI NA TUSIJIFANYE WAJUAJI SAAAANA KABLA YA KUMSIKILIZA MLALAMIKAJI.TUMSIKILIZE NA TUAMUE TOKANA NA USHAIDI KAMA UTAKUWEPO.HALAFU MKE HAIBIWI,NDOA NI MAKUBALIANO KATI YA WATU WAWILI WENYE HAKI SAWA NA AKILI TIMAMU.MKE ANAWEZA KUIBIWA TU KAMA NI BIDHAA,HANA MAAMUZI YA BINAFSI,NA ANAWEZA KUNUNULIWA NA KUUZWA NA KUMILIKIWA KAMA PROPERTY.KWENYE NDOA MNAYOSEMA SLAA SI MSHIRIKI WA MKATABA NA HIVYO HAWEZI VUNJA.WALIOKUBALIANA WAWILI NDIO WENYE UWEZO WA KUVUNJA NDOA.NA MKE KAMA SI BIDHAA,AU KAMA HANA MAAMUZI TIMAMU HAWEZI IBIWA.MUWE WAANGALIFU NA HOJA ZENU NA SIYO USHABIKI.

    ReplyDelete
  13. NDUGU ZANGU, UWE CCM AU CHADEMA.. IMEFIKIA WAKATI TUACHE KUPELEKESHWA NA MAWAZO YA UBINAFSI.. NCHI YETU INAHITAJI MABADILIKO TENA SIO MADOGO NA KWA HILO YEYOTE MWENYE AKILI TIMAMU NA AMBAYE HUWA ANARUHUSU UBONGO WAKE KUFIKIRIA OBJECTIVELY ATAKUBALIANA NA MIMI KUWA DOCTA SLAA NDIE PEKEE ANAYEWEZA KUTUONGOZA KULETA MABADILIKO KATIKA NCHI YETU, KWANI KABLA YA KUGOMBEA URAIS TUMEONA NI MAMBO GANI AMEIFANYIA NCHI YETU BILA WOGA NA KWA UZALENDO MKUBWA.. KUMBUKA TANZANIA SIO DAR ES SALAAM PEKE YAKE AMBAKO KUNA MAGOROFA NA BARABARA ZA DEZO esp. Masaki, KUNA WATU (MAJORITY) WANAISHI KATIKA UMASIKINI WA KUTISHA TANZANIA HII, Wanalala giza; Wanakosa hela (SH.100) ya kununulia koroboi. Wakati 'wawekezaji' wanasamehewa mabilioni ya kodi. WAMENYIMWA VINGI, TUWAACHE WAPIGE KURA KWA UHURU NA TUSIPINDISHE CHAGUO LAO..! Imenibidi niseme!

    ReplyDelete
  14. Watanzania tumechoshwa na CCM tumechoka,tumechoka na hatuhitaji tena kwanini CCM wanalazimisha kutuongo,jamani watanzania huu ni wakati wa mabadiliko hatutaki kuongozwa na vipofu wasiojali maslai ya watanzania. ebu angalieni jamani mkate mdogo ni sh 850,na mkubwa 1800,maisha yamekua magumu magumu mpaka basi tutafika kweli kwa hali hii? nawaomba watanzania tuungane kutetea nchii maana enaelekea pabaya. viongoz wa ccm hawatujali watanzania wanajali famlia zao na kulindana kutenda maovu tu ndani ya chama.miaka hamsini tuliwapa ya kutuongoza lakini hatujaona mababiliko kila kukicha hali inendelea kua ngumu zaidi, huu ni wakati wetu kuibadilisha nchi na kutetea haki zetu kwa njia yoyote bila kuogopa vitisho.

    ReplyDelete
  15. Matokeo yote aliyoyatolea Slaa, yale anayosema ni ya halali na yale anayodai yamebadilishwa yanasema kitu kile kile...Yeye KASHINDWA!

    ReplyDelete
  16. Hawa vibaraka wa CCM hawana jipya. Issue hapa ni kwamba WE HAVE TO DECIDE WHICH WAY TO TAKE. EPA, DECI, RICHMOND, UFUSKA ni ubinafsi ambao CCM na hasa viongozi wanataka kuutumia kuendelea kuwakandamiza wananchi. Bahati mbaya IQ ya viongozi wa CCM ni Sifuri. Hivi unategemea nini toka kwa MAKAMBA leo hii? Sasa neno AMANI lisitufanye tuache kufikiri. Kuna amani gani wakati kima cha chini ni shilingi 100,000 au dola 65? Rais mwenye mapenzi na huruma na wananchi atang'ang'ania mshahara wa 100,000. Ama kweli watanzania tumechoka kimawazo.

    ReplyDelete
  17. Tume ya uchabuzi ipo kwa ajili ya kuzuia watu wasipige kura fikiria vijana wa vyuo vikuu walivyozuiliwa, pia angalia idadi ya watu waliozuiwa kupiga kura eidha kwa majina kutokuwepo kwenye daftari au kwa kutokuwa na shahada ingawa jina lipo kwenye daftari. Vilevile angalia idadi ya waliopiga kura ni nusu au chini ya nusu ya watu waliojiandikisha na waliostahili kupiga kura hii ni aibu kwa tume, mimi naona Mzee Makame kesha choka hii kazi wanamlazimisha tu ili aisaidie CCM, lakini akumbuke kuwa kuifanya CCM ishinde kwa kutumia nguvu za dola na si nguvu ya umma ni kuwadangaya tu ipo siku watakuja kupotea na watu hawatawakuimbuka kamwe isipokuwa mwasisi wake tu, baba wa taifa marehemu J.K Nyerere maana alitaka CCM iwe chama cha wananchi ila waliopo wamekifanya kiwe chama cha wanyang'anyi wanaotembea kwenye kivuli cha chama cha wakulima na wafanyakazi

    ReplyDelete
  18. uchaguzi umekwisha tujenge inchi yetu,haya mambo ya nani kashinda na nani kashindwa hayatusidii kitu.u ccm na uchadema hauna nafasi sasa tunahitaji utanzania tu, ndio uliobaki.

    ReplyDelete
  19. nashauri dr. slaa achane na matokeo haya,sisi pia tunajua na tunazo taarifa za wizi. ni kweli matokeo yamechakachuliwa. Lakini tunaomba uende ukajenge chama, ili mwaka 2015 tuweze kushinda. Uendelee kuelimisha wananchi wasioelewa mabaya wanayotendewa na serikali ya CCM.

    ReplyDelete
  20. Hi Wa-Tz tumeonewa kweli na twaonekana wajinga wa hakuna mfano kabisa labda kwa kutupwa, tumefanyiwa kiini macho kabisa na hiki chama cha kupindua, yaani CCM, kama kweli ule mkutano wa Mwanza ulifanyika au haukufanyika wanajua wao lakini kilichoandikwa kwenye ule ujumbe mbona ndio CCM walivyofanya!!!!!!!!!!! Itakuwaje vi-tally? Hapa kuna jambo kabisa. Twaomba wa Tz wenye nia njema na nchi hii tuwe macho kabisa tunajua kuwa tumechelewa lakini tuwe macho tu na tuone ahadi zao zinafikia wapi. Sioni kama hata huyo rais ana raha na ushindi wake, kama wenzie walichakachua kura, ushindi ni wake binafsi sio wa maoni ya wananchi. Bwn. Slaa kaza buti tutafika tu, na wataumbuka, Mungu atusaidie!!!

    ReplyDelete