04 November 2010

Dkt. Shein aapishwa.

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

MAELFU ya wananchi wa Zanzibar, jana walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohammed Shein, zilizofanyika
Uwanja wa Amaan, Mjini Zanzibar.

Dkt. Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangazwa kuwa rais wa Zanzibar, Novemba Mosi mwaka huu na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), baada ya kupata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1 ambapo mpinzani wake Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), alipata kura 176,338 sawa na asilimia 49.1.

Wananchi hao, walianza kukusanyika katika uwanja huo kuanzia saa 12:00 za asubuhi ambapo sherehe hizo, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar na viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo Bw. Hamad, ambaye anakuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Sherehe hizo zimeandika histora mpya ya Zanzibar kutokana na wanachama wa vyama tofauti kukaa pamoja wakiwa wamevalia sare za vyama vyao na kushangilia pamoja bila kuwepo na malumbano yoyote.

Dkt. Shein aliapishwa saa 4:00 asubuhi na Jaji Mkuu wa Zanzibar Bw. Hamid Mahmoud. Akitoa shukrani zake Dkt. Shein alisema CCM imejizatiti kuunda Serikali ambayo itakidhi mahitaji ya wananchi, kulinda amani na utulivu uliopo visiwani humo.

“Napongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Aman Abeid Karume ambaye ameiacha Zanzibar ikiwa katika hali ya amani na utulivu hivyo jukumu lililopo mbele yetu ni kulinda amani hii ambayo imetokana na maridhiano yaliyofanywa na Rais Karume pamoja na Bw. Hamad,” alisema.

Baada ya kuapishwa, Dkt. Shein alikaguwa gwaride rasmi lililoandaliwa na Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, Vikosi vya SMZ na kupigiwa mizinga 21.

3 comments:

  1. BABU WAOLE MIKARAFUUNINovember 4, 2010 at 10:07 AM

    KIUKWELI MATAKEO YA UCHAGUZI ZANZIBAR YANALETA UTATA NA YANAONGEZA U
    MUHIMU WA KUWA NA TUME HURU YA UCHAGUZI.KIUKWELI MSHINDI ALIKUWA MAALIM SEIF LAKINI TUME YA UCHAGUZI ILISHINDIKIZWA KUTANGAZA MATOKEO BATILI.NI MATUMAINI YANGU KUWA MOJA YA MAMBO MUHIMU AMBAYO SERIKALI YA KITAIFA ITAFANYA NI KUHAKIKISHA INAJENGA MAZINGIRA YATAKAYORUHUSU UCHAGUZI HURU NA HAMILTON

    ReplyDelete
  2. Matokeo hayafutiki. wazanzibari waangalie kujenga nchi.Mwaka 2015 ni kesho.

    ReplyDelete
  3. Cha muhimu zaidi ni maendeleo ya ustawi wa jamii kwa wa ZANZIBARI WOTE bila kuangalia umweleo wa chama kama ilivyokuwa hapo awali.Imani kubwa ipo kuwa mipango ya kimaendeleo yatatekelezwa kwa vile serekali ya GNU itawashirikisha wazanzibari kikamilifu katika kuinua hali ya maisha,MIKARAFUUNI ikiwa ni moja ya mipango hiyo.

    ReplyDelete