*Yanga yaiua Toto African
*Ngassa awa shujaa wa Azam FC
Na Mhaiki Endrew, Songea
MABINGWA soka nchini, Simba jana waliendelea kung'ang'ania kileleni baada ya kuifunga Majimaji mabao 2-0 katika mechi ya
mwisho ya mzunguko kwanza ya Ligi Kuu Bara, iliyochezwa mjini Songea na kuifanya kuongoza kwa kuwa na pointi 27.
Wakati Simba ikiunguruma mjini, Songea wapinzani wao Yanga, nao waliwaangamiza ndugu zao Toto African mabao 2-0 ,katika mechi iliyochezwa Uwanja Jamhuri mjini Morogoro na kufikisha pointi 25, zilizoibakiza katika nafasi ya pili.
Bao la kwanza la Simba, lilifungwa dakika ya 81 na Jerry Santo, baada ya kukutana na mpira akiwa na nyavu na kuukwamisha mpira kimiani kirahisi.
Simba iliandika bao la pili dakika ya 88 na Emmanuel Okwi, ambaye aliichambua ngome ya Majimaji na kuachia shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja Majimaji, kama wachezaji wa Simba wangekuwa makini wangeweza kuondoka na lundo la mabao, baada ya washambuliaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' na Okwi kushindwa kutumbukiza mabao wavuni, baada ya kukosa mabao katika kipindi cha pili hasa, dakika ya 32 na 36.
Naye Nickson Mkilanya, anaripoti kutoka Morogoro kuwa Yanga nayo iliweza kuifunga Toto African, mabao 2-0 na kuendelea kubaki nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ambayo ilimaliza mzunguko wake wa kwanza.
Katika mechi hiyo, Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 26, kupitia kwa Nurdin Bakari, kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Toto, Wilbert Mweta huku timu hiyo ya Mwanza, ikikosa bao dakika ya 28 baada ya Lusango Meloo, kushindwa kutumbukiza mpira kimiani.
Kipindi cha pili Yanga, iliingia kwa uchu wa kutaka mabao na dakika ya 47, Nurdin tena aliiandikia timu hiyo bao la pili, baada ya kumchambua kipa Mweta wa Toto.
Kutoka Tanga, Speciroza Joseph anaripoti kuwa Azam FC jana iliifanyia kweli Ruvu Shooting, baada ya kuifunga mabao 4-1 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani.
Ruvu ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya 35, kupitia kwa Paul Ndauka baada ya kuwatoka walinzi wa Azam FC.
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kuliandama lango la Ruvu na kufanikiwa kupachika bao la kwanza dakika ya 47, kupitia kwa Mrisho Ngassa.
Azam ilipata bao la pili dakika ya 74 kwa mkwaju wa penalti uliowekwa kimiani na Ngassa, huku bao la tatu la timu hiyo likifungwa dakika ya 80 na Peter Senyonjo, aliyepokea pasi ya Jamal Mnyate.
karamu ya mabao ya Azam ilihitimishwa na Ngassa, ambaye jana alikuwa nyota wa mchezo dakika ya 88, baada ya kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.
No comments:
Post a Comment