11 November 2010

Salamu zamiminika kumpongeza Shein.

Na Mwandishi Wetu

SALAMU za pongezi kutoka ndani na nje ya Tanzania zinaendelea kumiminika kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa saba wa Zanzibar.

Salamu hizo za pongezi zinatoka kwa jumuiya, vyama vya siasa, vikosi vya ulinzi na usalama, mashirika, wizara, taasisi za serikali na zisizo za serikali, ofisi za ubalozi wa Tanzania zilizopo nje na ndani ya nchi pamoja na wananchi mbalimbali.

Miongoni mwa salamu hizo ni kutoka kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, ambayo imetoa salamu za pongezi kwa Dkt. Shein kwa ushindi wake alioupata katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Salamu hizo ziliendelea kutoa pongezi kwa kwa Dk. Shein kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuzingatia vyema sheria za nchi hasa sheria za uchaguzi na maadili ya vyama vya siasa, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Salamu hizo ziliendelea kueleza kuwa hekima na busara za Dkt. Shein zimeweka historia ya uchaguzi wa amani na utulivu hapa Zanzibar na kupelekea hata walioshindwa kukubali matokeo bila pingamizi zozote.

”Umeweka historia na msingi imara wa demokrasia hapa Zanzibar,” ilieleza sehemu ya salamu hizo.

Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza nao umetoa salamu za pongezi kwa Dkt. Shein na kueleza kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na chaguzi nyingine zilizofanyika Oktoba 31, ni hitimisho la wazi la kauli ya Wazanzibari kutaka kuimarisha umoja na mustakabali wao.

Nao Ubalozi wa Tanzania uliopo Geneva umetoa salamu za pongezi na kueleza kuwa una imani kubwa kuwa Dkt. Shein ataendeleza mema yote yaliofanywa na marais wa Zanzibar waliopita.

Ubalozi huo ulieleza kuwa unaamini kuwa kutokana na uzoefu wa Dkt. Shein, upendo alionao na uadilifu wake kwa watu wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla muungano utadumishwa.

Shura ya Maendeleo ya Waislamu Zanzibar nayo imepongeza kwa ushindi alioupata Dkt. Shein pamoja na CCM, katika uchaguzi huo.

Nacho chama cha The Tanzania Democratic Alliance Party (TADEA) kimetoa pongezi kwa Dkt. Shein na kumtakia mafanikio katika kuiongoza Zanzibar na kuahidi kuwa tayari kutoa ushirikiano katika kuijenga nchi hiyo na kudumisha amani na utulivu. 

Mtandao wa maendeleo wa Aga Khan (Aga Khan Development Network (AKDN) Tanzania na Zanzibar nao umetoa pongezi kwa Dkt. Shein na kueleza kuwa utaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali anayoingoza katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Aidha, salamu za pongezi zimetolewa na Afisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Dkt. Shein na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar, kwa kutambua uwezo wake pamoja na uadilifu, moyo wa kujituma na uzalendo wake, wameamua kwa moyo wa kimapinduzi kumchagua kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi awamu ya saba.

1 comment:

  1. eee si wameiba kura wapongezeni tu hao wafalme

    ReplyDelete