11 November 2010

Biashara ya chuma chakavu yaitesa TANESCO.

Na Patrick Mabula, Kahama

UONGOZI wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Tawi la Kahama limeiomba serikali wilayani hapa kuingilia kati uharibifu wa miundombinu ya nguzo za
umeme unaofanywa
na baadhi wa wananchi kwa kwa lengo la kujipatia vyuma chakavu.

Ombi hilo lilitolewa juzi na Meneja wa Tanesco wa tawi la Kahama, Bw. Sulle Khabati katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya, kikiwashirikisha viongozi wa vyama vya
siasa, mashirika mbalimbali ya umma, binafsi kwa lengo la kuwapongeza wale wote walioshiriki katika uchaguzi uliomalizika kwa amani na utulivu.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Khabati alisema kuwa kuna baadhi wa wananchi ambao kwa sasa wanajishughulisha na biashara ya vyuma chakavu ambapo nyakati za usiku hufanya uharibifu huo hasa katika nguzo za chuma  zinazopeleka umeme katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, hali ambayo inalitia hasara shirika na kuhatarisha maisha ya watu zinakopita nguzo hizo.

Meneja huyo alisema kuwa nguzo hizo ambazo hutoka katika kituo cha Ibadakuli mkoani Shinyanga hadi mgodi wa Buzwagi zimekuwa zikihujumiwa na watu hasa maeneo ya vijijini kutokana kwa kukatwa kwa baadhi ya vyuma vinavyoshikilia nguzo hizo na hivyo kufanya nguzo hizo kuzidiwa na uzito wa nyaya.

Bw. Khabati aliiomba serikali kuhakikisha kuwa inatafuta ufumbuzi wa suala hilo ambalo kwa sasa ni hatari kwa watu hususani wale wanaoishi kandokando ya nguzo hizo kama zikianguka kutokana na hujuma hiyo kwa vile zina umeme mkubwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja Mstaafu Bahati Matala alisema kuwa serikali itahakikisha inalifanyia kazi suala hilo na kuahidi kuwa pamoja na shirika hilo kulinda miundombinu hiyo na hivyo kutomuathiri mwekezaji huyo na kuhakikisha watu wanaofanya vitendo hivyo wanatiwa nguvuni na sheria kuchukua mkondo wake.

No comments:

Post a Comment