11 November 2010

Katibu asaini matokeo badala ya wagombea.

Na Eliasa Ally Njombe

ALIYEKUWA mgombea ubunge Jimbo la Njombe Kaskazini Kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Alatanga Nyagawa
amemtuhumu Katibu wa chama hicho wa Wilaya ya Njombe, Bw. Benedict Mligo kupokea rushwa na kusaini matokeo ya uchaguzi badala ya wagombea.
 
Kutokana na sababu hiyo, Bw. Nyagawa amesema anatarajia kwenda mahakamani kupinga matokeo ambayo yalionesha kuwa Bw. Deo Sanga wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alishinda kwa kura 29,644 dhidi yake aliyeambulia kura 6,781.
 
Mgombea wa CHADEMA Nyagawa alisema kuwa anamshutumu katibu huyo kuwa alipewa sh. 500,000 ili asaini matokeo. huku akijua kuwa wagombea wake hawakukubaliana nayo.
 
“Mimi sikubaliana na matokeo hayo wala sitomkubali mgombea aliyetangazwa kwani haiwezekani katibu akasaini fomu ya tangazo au hati ndogo inayojulisha nani ameshinda
bila kukubaliana na mgombea wala chama.

"Hii ni kukisaliti chama, kwani inadaiwa walipewa fedha huku akiwa ni kiongozi ambaye anategemewa na kuaminiwa wanachama wa CHADEMA, lakini hakuwasiliana na mgombea na kumkubalia kusaini matokeo,” alihoji Mgombea.
 
Alisema msimamizi wa uchaguzi alitumia udhaifu wa viongozi hao ambao hawana msimamo wala mamlaka ya kufanya hivyo, kutoa maamuzi kuwa mgombea wa CCM ameshinda.
 
“Sisi tulipata taarifa kuwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Bw. Mkupete alimpigia simu moja kwa moja Mligo kwamba aende akasaini wakati wagombea anawajua,” alisema Bw. Nyagawa.
 

Alisema kuwa atakwenda mahakamani na atamkubali mgombea aliyepita kwa kuwa amefanyiwa njama kumwangusha katika uchaguzi huo.
 
Akijibu tuhuma hizo, Bw. Mligo pamoja na kukiri kusaini matokeo, alisema hakupokea hongo kufanya hivyo,  bali aliambiwa na msimamizi wa uchaguzi asaini
fomu na siyo matokeo ya mgombea wa CHADEMA.

"Mimi nilijua kuwa ni tangazo tu la kawaida ambalo vyama vyote vinatakiwa tusaini, sikuelewa kama nilichosaini kama yalikuwa ndiyo matokeo ya kura, mambo hayakuwekwa
wazi, na ningejua kuwa ni matokeo nisingeyasaini kwa kuwa utaratibu nauelewa fika," alisisitiza Bw. Chapwila.

Pia aliyekuwa mgombea ubunge wa Njombe Magharibi (CHADEMA), Bw. Thomas Nyimbo alisema kuwa hata yeye alishangaa kwa nini katibu yule alikubali kusaini bila kuwasiliana na wagombea,

"Nilimuuliza yule katibu wangu nani alikuruhusu kusaini, alinijibu nimsamehe eti yeye hakuelewa na akasaini kwa hivyo hata ukimlaumu haisaidii,” alisema.

1 comment:

  1. huo ni usailiti na adhabu ya usaliti ni kifo,ndugu zangu wakati umefika wa kuchukua hatua kwa wasaliti kwani hata yuda eskariot baada ya kumsaliti bwana yesu alichukua uamuzi,nashauri huyo katibu achukue uamuzi kabla hatujamchukulia uamuzi anaositahili.

    ReplyDelete