03 November 2010

Rais Zuma apangua baraza la mawaziri.

JOHANESBURG,A.Kusini.


RAIS wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ameonesha uwezo wake wa  madaraka  kwa kupangua mawaziri saba katika baraza lake,mabadiliko ambayo wakosoaji wa
masuala ya kisiasa wanasema kuwa ni makubwa katika historia ya  baraza la mawaziri nchini humo.

Mabadiliko hayo yanadaiwa kuwa ni ya kwanza nchini humo kutokana na kuwa tangu umalizike utawala wa kibaguzi nchini humo miaka 16 iliyopita, hakuna baraza la mawaziri lililowahi kupanguliwa kama alivyofanya Rais Zuma Jumapili iliyopita tangu akiwemo kiongozi aliyemrithi Rais Thabo Mbeki.

Rais Mbeki amewahi kukataa kumtimua kazi Waziri wa Afya, Bi.Manto Tshabalala-Msimang ambaye alihimiza dawa za kupunguza makali ya maradhi ya UKIMWI kama dawa ya kutibu baada  ya kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Mbali na kiongozi huyo,pia Rais Nelson Mandela naye alikalia kiti moto akishinikizwa kumfukuza kazi Waziri wa Elimu,  Bw.Sibusiso Bhengu ambaye alikuwa akishutumiwa kwa matokeo mabovu katika shule nchini humo.

Mmoja wa wachunguzi wa masuala ya kisiasa,  Bi.Susan Booysen kutoka Chuo Kikuu cha  Witwatersrand aliyaita mabadiliko hayo ni hatua ya Rais Zuma kujaribu kuficha sura yake ya uongozi wake dhaifu.

“Mbeki kamwe hakuwa na nia ya kufanya mabadiliko na badala yake anazitumia nafasi za uwaziri kama bima kisiasa kwa ajili ya kuonesha  utii,”amesema.

Hata hivyo vyombo vya habari nchini humo vimempongeza Rais Zuma kwa hatua yake hiyo ya kupangua baraza la mawaziri huku gazeti la Times likisema kuwa amevunja kipengele ambacho kimekuwa kikikandamiza demokrasia ya Afrika Kusini kwa muda wa miaka 16.

Wakati Times likisema hivyo, gazeti la  The Star limesema kuwa kiongozi huyo amechukua hatua hiyo ili kupambana na viongozi wasio kuwa watendaji.


Habari kutoka nchini humo zimeeleza kuwa miongoni mwa mawaziri waliopitiwa na panga la Rais Zuma,ni Waziri wa Mawasiliano, Bw. Siphiwe Nyanda,ambaye alikuwa Mkuu wa Ulinzi na kiongozi mwandamizi katika chama tawala cha African National Congress ambaye alizua zogo baada ya kumfukuza kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu katika wizara hiyo baada ya kuibua shutuma za rushwa dhidi ya kiongozi huyo.


Mbali na Waziri huyo,vilevile Rais Zuma amemtimua kazi Waziri wa Wanawake,Watoto na wenye ulemavu, Bi.Noluthando Mayende-Sibiya,ambaye anaonekana kufukuzwa kutokana na safari za kifahari huku akishindwa kuandaa progaramu kwa ajili ya Wizara hiyo mpya.

Inaelezwa kuwa pamoja na kujaribu kuongeza chachu katika utendaji,mabadiliko hayo pia yanadaiwa ni ya kurejesha umoja miongoni wafanyakazi wenye msimamo wa mlengo wa kushoto na Umoja wa Vijana wa ANC ambao ndiyo waliompandisha chati katika uchaguzi uliopita.

“Amejaribu kutumia madaraka yake kama rais kwa kuwaonesha wananchi kwamba anasikitishwa na utendaji mbovu wa baadi ya mawaziri,”alisema  Prince Mashele ambaye ni mchambuzi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Usalama iliyopo mjini  Pretoria.

Miongoni mwa waliopandishwa vyeo ni Mkuu wa zamani wa Umoja wa Vijana, Bw. Fikile Mbalula ambaye alisaidia kampeni ambazo zilifanya kushuhudiwa Rais  Zuma mwaka 2007 akichaguliwa kuwa Rais wa chama cha ANC.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Polisi kwa sasa amechaguliwa  kuwa Waziri wa Michezo.

Kupandishwa cheo Waziri huyo inaelezwa kuwa itaondoa malumbano ya ndani kwa ndani kati ya chama na umoja wake wa vijana ambao umekuwa ukimpinga wazi Rais Zuma kuhusu masuala mbalimbali likiwemo la migodi na pia mahusiano binafsi ya Rais Zuma na wakeze na wanae.

No comments:

Post a Comment