03 November 2010

Aliyeteketeza Watutsi Kanisani atupwa jela.

KIGALI,Rwanda

MFANYABIASHARA mashuhuri nchini Rwanda amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kushiriki kuteketeza Kanisa ambalo lilikuwa
limehifadhi watu zaidi ya 2,000 wa kabila la Watutsi wakati wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Habari kutoka nchini humo zilieleza kuwa mfanyabiashara huyo,Bw. Gaspard Kanyarukunga (65) alihukumiwa kifungo hicho juzi baada ya Mahakama maalumu ya Umoja wa Mataifa (UN) kumkuta na hatia ya mauaji ya halaiki na ukiukaji wa haki za binadamu.


Msemaji wa mahakama hiyo alisema kuwa Bw. Kanyarukiga alikutwa na hatia ya kuwakusanya kwenye makundi ya  Watutsi ndani ya Kanisa kabla ya kuita watu kulitia kiberiti ingawa mtuhumiwa huyo anakana mashtaka hayo.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa mwezi Julai mwaka 2004 nchini Afrika Kusini na kusafirishwa hadi Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia mauaji ya Rwanda (ICTR) yenye Makao yake Makuu mjini Arusha Tanzania.

Mtuhumiwa huyo anakuwa wa pili kuhukumiwa kwa mauaji  ya watu ndani ya Kanisa hilo la Notre Dame de la Visitation lililopo katika eneo la  Nyange baada ya aliyekuwa kiongozi wa Kanisa hilo,Bw.Athanase Seromba kuhukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment