11 November 2010

NHC kujenga nyumba milioni 3.

Na Jovin Mihambi, Mwanza

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limepanga kuwekeza zaidi katika ujenzi wa nyumba milioni tatu ili kukidhi mahitaji ya wapangaji wake wa sasa na
wale ambao watakaojitokeza baadaye.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtandaji wa shirika hilo, Bw. Nehemiah Mchechu alipokutana na wapangaji wa shirika hilo jijini Mwanza katika
ukumbi wa Hoteli ya La Cairo.

Alisema katika kutekeleza azima hiyo ya kujenga nyumba milioni tatu, NHC itahakikisha inafanya hivyo kwa taratibu, ikiwa ni pamoja na kupanua wigo kwa kujenga magorofa sehemu mbalimbali za wilaya nchini kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wapangaji wake.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo alisema shirika lake linatarajia kujenga nyumba 15,000 ndani ya miaka mitano ijayo, kwa ajili ya kupangisha Watanzania, wakiwemo wafanyabiashara kwa ajili ya biashara, kuanzia ghorofa moja kwenda juu.

Alisema dhamira hiyo imelenga kuboresha zaidi shirika hilo ambalo ni kubwa kuliko yote kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, na kwamba NHC inatarajia pia kuuza baadhi ya nyumba zake ambazo hazikidhi viwango kwa wapangaji wa kizazi cha sasa.

Mkurugenzi huyo alisema katika mkakati huo wa ujenzi wa nyumba 15,000 utasaidia maradufu Watanzania kupata fursa ya kupanga na kuendesha shughuli zao, hivyo kuleta tija na maendeleo kwa taifa.

"NHC tumepanga kujenga jumla ya nyumba 15,000 kwa miaka mitano ijayo. Lakini zipo baadhi ya nyumba zetu tutaziuza kwa wapangaji na kujenga nyingine nzuri zaidi," alisema Bw. Mchechu.

Aidha, Mchechu alitoa onyo kwa Watanzania wanaowazunguka na kuwanyang'anya wajane nyumba walizoachiwa na waume zao, na kwamba yeyote atakayebainika kufanya hivyo hatavumiliwa.

No comments:

Post a Comment