*Aitungua Harambee Stars.
Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya
Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', Jan Poulsen amemsifu mfungaji wa bao hilo, Gaudance Mwaikimba kwa kusema ndiye aina ya mshambuliaji anayemuhitaji.
Mwaikimba alifunga bao hilo pekee dakika ya kwanza kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngassa, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Poulsen mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, alisema ana imani Mwaikimba atazidi kuonesha makali yake kutokana na jinsi anavyocheza na kuutumia vizuri mwili wake bila kuogopa.
"Nimeridhishwa na kiwango cha Mwaikimba, kwani ni mchezaji mzuri mwenye nguvu na anautumia vizuri urefu wake, nina imani ningemuona mapema katika mchezo dhidi ya Morocco angeisaidia safu ya umaliziaji kutokana na mipira mingi ya juu kupotea," alisema Poulsen.
Akizungumzia mchezo huo, Poulsen alisema walicheza vizuri katika dakika 20 za kwanza, lakini mchezo ulibadilika kutokana na Harambee Stars nao kubadilisha aina ya uchezaji, lakini anashukuru wameshinda.
Katika mchezo huo wa jana, timu zote zilianza kwa kasi na kushambuliana kwa zamu ambapo mpaka dakika 45 za kwanza Kilimanjaro Stars, iliongoza kwa bao lililofungwa na Mwaikimba dakika ya kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko ambapo Kili Stars, iliwatoa wachezaji sita kwa mara moja na Harambee Stars nao ilitoa wawili.
Mchezaji Salum Machaku wa Kili Stars aliyeingia badala ya Idrissa Rajabu, nusura aifungie Stars bao la pili baada ya wachezaji wa timu hiyo kuonana vizuri, lakini shuti lake lilipaa juu ya goli.
Harambee Stars ilijibu shambulizi hilo dakika ya 85 kutpitia kwa Bob Mugayia, aliyeingia badala ya George Odhiambo kupiga shuti dhaifu lililotua mikononi mwa kipa, Juma Kaseja akiwa eneo la hatari.
Hongereni sana Kilimanjaro stars, huo ni mwanzo mzuri, wachezaji mzidishe bidii katika michezo inayofuatia na Mungu atawabariki. Watanzania wapendao mchezo wa mpira nina imani watakuwa pamoja nanyi siku zote za michezo.
ReplyDelete