Na Elizabeth Mayemba
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya michuano ya Kombe la CECAFA Tusker Chalenji, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi.
Akitangaza viingilio hivyo Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Sunday Kayuni, alisema viingilio vya mechi zitakazochezwa Uwanja wa Taifa vitakuwa sh. 20,000 kwa VIP A, VIP B sh. 15,000 VIP C sh. 10,000, viti vya rangi ya machungwa sh. 7,000, bluu sh. 5,000 na viti vya kijani sh. 3,000.
Kayuni alisema Uwanja wa Uhuru viingilio kwa viti maalumu kitakuwa sh. 10,000, jukwaa kuu sh. 7,000, la kijani sh. 5,000 na mzunguko kitakuwa sh. 2,000.
Ufunguzi wa michunao hiyo utafanyika Jumamosi katika Uwanja wa Taifa Stars itacheza na timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo'.
"Tumeweka viingilio vya chini, ili kila mmoja aweze kumudu kwenda kuangalia michuano hii, kwani pia itasaidia watu kuingia kwa wingi uwanjani," alisema Kayuni.
Akizungumzia maandalizi ya michuano hiyo, Kayuni alisema kila kitu kinakwenda vizuri na timu zote zilizotajwa hakuna hata moja iliyoahirisha na leo Somalia itakuwa timu ya kwanza kufika.
Kayuni alisema kwa upande wa timu ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', inaendelea vizuri na mazoezi na tayari wachezaji wake watatu wanaocheza soka la kulipwa wamejiunga na wenzao, ambao ni Henry Joseph, Idrissa Rajabu na Thomas Ulimwengu.
Alisema mchezaji, Nizar Khalfan anatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote lakini Danny Mrwanda, timu yake imeweka kambi mbali, hivyo kuanzia Jumapili ijayo atakuwa huru na kocha, ndiye atakayeamua kama atamwita tena au la.
Wakati huo huo, Kayuni alisema watu 64 wamejitokeza kuomba nafasi ya Katibu Mkuu wa TFF na 44 katika nafasi ya Ofisa Habari.
Alisema tayari wameshafunga maombi kilichobaki ni watu walioomba nafasi hizo na kutimiza vigezo wataitwa kwa ajili ya kufanyiwa usaili, kwani wanataka mpaka kufikia Desemba 15 mwaka huu, Katibu Mkuu na Ofisa Habari wawe wameshapatikana.
No comments:
Post a Comment