24 November 2010

China,A.Kusini zaiwania Zimbabwe.

HARARE,Zimbabwe.

HUKU  upande mmoja China na Afrika Kusini zikiimarisha uhusiano wao, kwa upande mwingine nchi hizo zinaripotiwa kuwa zipo kwenye kinyang'anyiro cha kuidhibiti Zimbabwe kwa
mtazamo wa kunufaika zaidi na maliasili za nchi hiyo, yakiwemo madini

Hivi karibuni, Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini alimualika Makamu wa Rais wa China, Bw.Xi Jinping, nchini mwake ambaye ndiye anayetarajiwa kuchukua hatamu ya uongozi nchini mwake na Rais  Zuma akatumia fursa hiyo kusaini naye mikataba ya kuboresha biashara baina ya nchi zao, huku China ikionekana kulenga kuwekeza zaidi nchini Afrika ya Kusini.

Hata hivyo inaelezwa kuwa unapovuka mpaka na kuingia Zimbabwe, washirika hao  wanatizamana kwa jicho la uhasama.

Inaelezwa kwamba kwa miaka kadhaa sasa, mataifa hayo mawili yamekuwa yaking'ang'ania kudhibiti na kuwa na usemi zaidi katika uchimbaji wa madini na raslimali nchini Zimbabwe.

Inadaiwa kwamba awali taifa hilo, lililoko katika kanda ya Afrika Kusini, lilikuwa na usemi mkubwa kutokana na mali asili yake na lilinawiri pia katika sekta ya kilimo kabla ya serikali ya Rais Robert Mugabe kuanza kulivuruga na kusababisha mfumko wa asilimia milioni 500 wa bei kwenye uchumi wake mwaka  2008.

Thamani ya mauzo ya bidhaa za Afrika Kusini nchini Zimbabwe ni kama asilimia 20 ya pato la ndani la Zimbabwe huku m saada wa China kwa taifa hilo lililowekewa vikwazo vya kiuchumi kutokana na ukiukaji wake wa haki za binadamu, umemsaidia Rais Mugabe na chama chake tawala cha ZANU-PF kustahimili balaa ya kutengwa na jumuiya ya kimataifa.

Inadaiwa kwamba pamoja na misaada hiyo,China na Afrika ya Kusini zinanuia kudhibiti migodi mikubwa zaidi duniani ya madini ya Platinum inayokadiriwa kuwa yenye thamani ya mabilioni ya Dola, almasi na pia utajiri wa kilimo na pia kuwa na usemi katika hazina ya takriban dola bilioni 10 ya maendeleo ya kulijenga upya taifa hilo baada ya utawala wa Rais Mugabe kuisha na sera ya demokrasia kuwepo.

Anne Fruhauf, ambaye ni mchambuzi wa  masuala ya uchumi katika kundi la Eurasia, anasema mataifa hayo mawili yakilinganishwa kwa sasa, Afrika kusini imejitokeza waziwazi katika maazimio yake ya kiuchumi baada ya kuwekeza katika sekta ya uchimbaji madini na biashara ya benki.

Mataifa mengine ambayo yamekuwa yakilenga kuwekeza na kuidhibiti Zimbabwe kibiashara ni mtawala wake wa zamani, Uingereza, na pia India ambayo kampuni yake ya Essar hivi karibuni ilisaini mkataba wa kuendesha biashara ya kuchonga vyuma wenye thamani ya Dola milioni 500.

Hata hivyo inadaiwa kuwa kinyang'anyiro hicho cha udhibiti kinaweza kumpa Bw Mugabe nafasi ya kulipuuza taifa moja na kuliangazia lingine na hatimaye awe na nguvu zaidi ya kuwakashifu wakosoaji wa magharibi na pia kuwakandamiza wapinzani wa ndani wa kisiasa.

No comments:

Post a Comment