04 November 2010

Mpangala aishauri Serikali.

Na Amina Athumani

SERIKALI imetakiwa kuisaidia Kamati ya Miss Tanzania katika maandalizi ya mshiriki wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, ili aweze kufanya
vizuri kwenye michuano hiyo ya urembo.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na baba mzazi wa Miss Tanzania 2010, Genevieve Emmanuel, Emmanuel Mpangala alipofika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumpokea mtoto wake ambaye alikuwa akiwasili akitokea China, katika mashindano ya Miss World yaliyofanyika wiki iliyopita.

Mpangala alisema Kamati ya Miss Tanzania, inatakiwa kupewa sapoti na Serikali katika maandalizi ya mrembo wa Tanzania, kabla ya kwewnda kushiriki michuano hiyo kwa kuwa uhaba wa wadhamini ndiyo unaosababisha mrembo kuandaliwa kwa muda mfupi.

"Kwa kweli mimi nimefuatilia kwa makini sana mashindano ya Miss World na nimegundua sisi tunatakiwa kumuandaa zaidi mrembo wetu kwa kipindi kirefu kidogo na si mwezi mmoja, kama ilivyo sasa hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha inaunganisha nguvu za pamoja na Kamati ya Miss Tanzania, ili mrembo atakayeweza kuiwakilisha nchi awe amepewa maandalizi ya kutosha.

"Mfano mrembo wa Kenya alikuwa na data nyingi za kijamii na hii imetokana na maandalizi ya kutosha waliomfanyia mrembo wao kwa mfano Ginevieve, alifanya tukio moja tu la kutembelea wagonjwa wa matende hivyo matukio kama hayo, mrembo anatakiwa ayafanye mengi kabla ya kushiriki michuano hii," alisema Mpangala.

Naye Genevieve alisema ameshukuru kwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya Dunia na kwamba mengi zaidi na changamoto alizoziona, atazinzungumzia katika mkutano wa pamoja, utakaoandaliwa na Kamati ya Miss Tanzania.

Hii ni mara ya 17 kwa Tanzania kushiriki kinyang'anyiro hicho, tangu mwaka 1994 ambapo mwaka 2005, Nancy Sumary alifanikiwa kutwaa taji la Miss Afrika World.

No comments:

Post a Comment