*Bingwa kuzoa mil. 45/-
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', imepangwa kuanza na Zambia katika michuano inayoandaliwa na Baraza la Vyama
vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Kwa mujibu wa ratiba ya CECAFA, mashindano hayo yamepangwa kufanyika kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam yakiwa katika makundi matatu, huku Kundi B likiwa na timu za Rwanda, Ivory Coast, Sudan na Zanzibar likionekana kuwa gumu.
Mbali na kutolewa ratiba, pia CECAFA ilitangaza zawadi kwa washindi ambapo bingwa wa mashindano hayo anatarajia kuzoa kitita cha dola 30,000 (sh. milioni 45), wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa baraza hilo Leodegar Tenga alisema maandalizi ya mashindano hayo, yamekamilika kwa kiasi kikubwa kwani wadhamini wameendelea kukamilisha baadhi ya vitu.
Alisema mashindano hayo, sasa wanafikiria yafanyike katika mikoa miwili tofauti na awali, ili Watanzania wengi wapate ladha na si kufanyika sehemu moja tu, Dar es Salaam.
"Kama utaangalia ratiba yetu sehemu ya uwanja hatujaweka mpaka sasa, hiyo imetokana na kutojua kama tutakuwa na uwezo wa kutumia viwanja viwili katika mikoa tofauti, tulipanga kundi moja liende Mwanza na makundi mawili yabaki Dar es Salaam.
"Kikubwa kinachotukwamisha ni fedha, kama tutapata mdhamini mwingine, mbali ya huyu tuliyenaye hakuna shaka kundi moja litakwenda Mwanza, tutakutana Kamati ya Utendaji pamoja na viongozi wa Mwanza, kujadili suala hili kwa kina, tunataka watu wa mikoani nao washiriki," alisema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Richards Wells ambayo ndiyo wadhamini wa mashindano hayo, alisema kampuni yake itahakikisha kila timu inayoshiriki inapatiwa huduma nzuri.
Alisema kwa mwaka huu, wametenga dola 60,000 katika zawadi ikiwa ni sehemu ya udhamini wa dola 450,000 ambapo bingwa atajinyakulia dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.
Wakati Kilimanjaro Stars ikifungua pazia na Zambia kundi A, timu zingine za kundi hilo Burundi na Somalia pia zitaumana siku hiyo.
Kundi C lina timu za Uganda, Kenya, Malawi na Ethiopia ambapo Novemba 29, Ethiopia itaumana na Uganda na Malawi itacheza na Kenya, kundi B Sudan itacheza na Zanzibar na Rwanda itaoneshana kazi na Ivory Coast Novemba 28.
Timu mbili zitakazofanya vizuri katika kila kundi, zitaingia robo fainali pamoja na mbili zenye matokeo mazuri, ambapo robo fainali itaanza Desemba 7, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment