Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WAGOMBEA ubunge katika majimbo ya Shinyanga mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na jimbo la Maswa
Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wametangaza rasmi adhima yao kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
Katika Jimbo la Shinyanga Mjini, mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, Bw. Philipo Shelembi anakusudia kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyomtangaza mgombea wa CCM, Bw. Steven Masele kuwa ndiye mshindi kwa kupata kura 18,750 dhidi ya 18,507 alizopata mgombea huyo wa CHADEMA.
Huko katika jimbo la Maswa Mashariki, Bw. Peter Bunyongoli anakusudia kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mgombea wa CHADEMA, Bw. Sylivestar Kasulumbai kwa kura 17,075 dhidi ya 17,014 za Bw. Bunyongoli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini , Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Nyangaki Shilungushela alisema hivi sasa wanawasiliana na wanasheria wao
ili kuandaa taratibu za kupinga matokeo hayo mahakamani.
Bw. Shilungushela alisema sababu kubwa iliyosababisha chama chake kikate rufaa ni jinsi msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Bw. Festo Kang’ombe alivyopindisha matokeo halali ya kura na kuamua kumtangaza mgombea wa CCM ambaye matokeo yote katika vituo vya kupigia kura yanaonesha wazi alishindwa.
“Tayari tunawasiliana na wanasheria wa chama chetu, Bw. Mabere Marando na Tindu Lissu ili waweze kuandaa taratibu za kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Shinyanga Mjini, matokeo yalipotoshwa, siyo halali.
“Kwa mujibu wa matokeo kutoka katika vituo vya kupigia kura mgombea wetu wa CHADEMA ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo, lakini ajabu aliyetangazwa ni mgombea wa CCM, hata hivyo mpaka hivi sasa msimamizi ameshindwa kutangaza idadi kamili ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo, maana wamechakachua,†alieleza Bw. Shilungushela.
“Matokeo haya sisi yametupa wasiwasi mkubwa kuwa kuna uchakachuaji wa hali ya juu uliofanyika kwani ndani ya chumba cha kujumlishia kura msimamizi alidai mgombea
wa CCM alishinda kwa tofauti ya kura moja, lakini CCM wanadai mgombea wao alishinda kwa tofauti ya kura 39.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika jimbo la Maswa Mashariki, Bi. Elizabeth Kitundu alisema mgombea wa CCM, Bw. Peter Bunyongoli alikuwa anakusudia kukata rufaa kupinga matokeo katika jimbo hilo.
Bi. Kitundu alisema mgombea huyo analalamikia matokeo katika kata tatu ambako alidai kura zake ziliibwa na hivyo anakusudia kupinga matokeo hayo.
Mgombea huyo wa CCM alikiri kulalamikia matokeo hayo kwa kudai kuwa baada ya kubaini mapungufu katika kata tatu aliomba kurejewa kuhesabiwa kwa kura lakini msimamizi alikataa.
Pamoja na hali hiyo, Bw. Bunyongoli alikanusha madai ya kutaka kukata rufaa yeye mwenyewe kwa kusema kwamba tayari amewasiliana na viongozi wa CCM ngazi za juu ambao wao wenyewe ndiyo watakaoamua iwapo wakate rufaa au wasikate.
No comments:
Post a Comment