21 November 2010

Majambazi yamiminia risasi basi, yaua abiria.

*Polisi watupa bunduki kwa kuogopa
*Basi laharibiwa, abiria 23 wajeruhiwa


Na. Prosper Kwigize, Kibondo.
MAJAMBAZI nane wakiwa na silaha za kivita wameshambulia na kuteka gari la abiria na kusababisha kifo cha abiria mmoja na wengine kujeruhiwa kabla ya kupora mali mbalimbali za
abiria pamoja na bunduki mbili za polisi waliokuwa wamesindikiza basi hilo.

Tukio hilo limetokea lilitokea jana katika eneo la Mukugwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma kilomita takribani 30 kabla ya kufika  mjini Kibondo, ambako majambazi hayo yalilishambulia basi la kampuni ya Golden Inter City Express lenye namba za usajiri T457 ACR linalofanya safari zake kati ya Kigoma na Mwanza.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kibondo, Bw. Dan Makanga ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, majambazi hao hawakuweka kizuizi chochote na kwamba waliibuka kutoka porini na kuanza kurusha risasi mfululizo na kuharibu vibaya basi hilo.

“Majambazi wanne wakiwa na silaha nzito walijitokeza barabarani na kuaanza kurusha risasi hali iliyomlazimu dereva wa basi hilo Bw. Method Chang’a kulisimamisha, wakatoa amri kwa askari polisi waliokuwemo ndani ya basi hilo kusalimisha silaha na kadri walivyochelewa kufanya hivyo  ndivyo majambazi hao walivyozidi kupiga risasi sehemu mbali  mbali na kusababisha abiria wengi kujeruhiwa na risasi hizo,”  alisema mkuu huyo wa Wilaya ya Kibondo.

Imeelezwa kuwa kutokana na kuendelea kupigwa kwa risasi hizo kwa fujo huku askari polisi nao wakijaribu kujihami na kuwalinda abria bila mafanikio, walilazimika kuzirusha nje ya basi bunduki zao kitendo kilichowapa fursa majambazi kuliteka na kuanza kupora abiria mmoja baada ya mwingine.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Dkt. Florian Ntinuga alisema kuwa abiria aliyeuawa ni Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM Musoma Vijijini mkoani Mara Bw. Wilfred Peter Muga na abiria 23 wamejeruhiwa na kufikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo. Watatu kati yao hali zao ni mbaya na watasafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa Bungando mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi.

Majambazi hao ambao hawakuwa wameficha sura zao waliweza kutokomea porini bila kukamatwa huku wakiondoka na silaha mbili aina ya SMG zikiwa na magazine nne mali ya Jeshi la Polisi na msako mkali katika pori hilo unaendelea ili kuwatia mbaroni majambazi hayo.

Eneo la Mkugwa lilipotokea tukio hilo lilikuwa kambi ya wakimbizi mchanganyiko kabla ya kufungwa na wakimbizi hao kuhamishiwa wilayani Kasulu na eneo hilo kufunguliwa
shule ya sekondari ya wasichana.

Hili ni tukio baya la pili kutokea eneo hilo.  Miezi minne iiliyopita majambazi yalilitega gari dogo la abiria na kumuua mwalimu Deo Kato ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Parokia ya Kanisa Katoliki Kibondo akiwa njiani kutoka Kasulu kwenda Kibondo.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, George Mayunga hazikufanikiwa kutokana na simu yake kuwa katika matumizi kwa  muda mrefu.

Hata hivyo Mkuu wa Polisi wilayani Kibondo,  Innocent Rwelamira amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa askari wawili waliokuwa na silaha aina ya SMG wakisindikiza basi hilo wameporwa silaha zao na kujeruhiwa.

3 comments:

  1. watz mnachekesha, eti askari wanasindikiza/wanalinda bus nao wamekaa ndani ya bus. hatuko wabunifuu, kitu cha kwanza mawasiliani ni muhimu, ili askari wapate support wanapozidiwa, labda tulete wawekezaji hata ktk hilo!!!!!????? hahahah

    ReplyDelete
  2. tukiwa wazalendo ni vizuri kutoa maoni yanayotekelezeka na wala siyo kulaumu.kila kitu kina mipangilio na mikakati yake.
    mi nashauri polisi ikae na serikali kuu ili kupanga namna ya kutatua tatiazo hili.
    mfano;magari ya uhakika yenye mawasiliano yawepo
    pili,sehemu hizo ziwekwe kama operesheni.yaani askari wakae kwa mwezi au miezi itategemea makubaliano ya wapangaji.
    tatu,wanachi wazungukao sehemu hiyo washirikishwe kutambua wahalifu au wageni.
    nne'wakati mwingine nchi ya jirani ishirikishwe kwani siyo ajabu ni wale wakimbizi waliokaa hapo miaka ya nyuma wanaojua mazingira ya pori hilo ndo wanarudi kiaina.
    kwa hapo mim nina hakika kabisa hao majabazi yatatokomea.
    siyo kukaa kulaumu kila siku wakati tujua ulizi ni ya wote.muulize mwema ulinzi shirikishi . mimi nimepitia JKT. nikipewa hiyo kazi naweza.

    ReplyDelete
  3. Kuwe na ulinzi unaoonekana kila siku katika sehemu ambazo zimekuwa na ujambazi wa namna hii. Kama italazimu hata kujenga vituo vya polisi wanaolinda mapoli wanamojificha majambazi. Kama Mkuu wa Wilaya na watendaji kazi wake hawawezi kazi ya ulinzi na usalama wa Wananchi, wanaombwa waache kazi. Usalama wa Wananchi ndiyo kazi namba moja ya serikali katika ngazi zote.

    ReplyDelete