21 November 2010

Mapambano yetu ya kudumu-Mbowe.

*Asisitiza katiba mpya, tume ya uchaguzi na ya uchunguzi

Na Tumaini Makene.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa mapambano ya kudai katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na tume huru ya kuchunguza kilichojiri katika
uchaguzi mkuu uliopita, yatakuwa ya kudumu mpaka yatakapofanyiwa kazi na mamlaka husika.

Kimesema kuwa kinadai masuala hayo kwa maslahi ya mamilioni ya Watanzania nchini kote, bila kujali dini, kabila, rangi wala chama, ambao wangependa kuona nchi ikiingia katika uchaguzi mwingine miaka mitano ijayo ikiwa tayari na tume huru ya uchaguzi, pamoja na katiba mpya au walau mchakato wake ukiwa umeanza.

Akizungumza na Majira Jumapili jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema "haya yatakuwa mapambano ya kudumu mpaka kitakapoeleweka, tunaomba watu watuelewe, tumeamua kudai vitu hivi kwa njia za kidemokrasia na amani, kama tulivyofanya juzi bungeni.”

Bw. Mbowe pia alisema kuwa kitendo cha wabunge wa chama hicho kutoka bungeni wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kutoa hotuba ya kulifungua bunge, kilikuwa cha kidemokrasia, kilichopeleka ujumbe mzito kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa, ili kuibua mjadala wa kitaifa juu ya umuhimu wa masuala hayo matatu.

"Watu wasipotoshe hatuna chuki binafsi na Rais Kikwete, suala si kumtambua au kutomtambua...tunataka kupeleka ujumbe mzito unaoibua mjadala juu ya mambo ya msingi kwa nchi hii, madai yetu ya msingi ni matatu tu; tume huru ya uchaguzi, katiba mpya na tume huru ya kuchunguza uchaguzi mkuu uliopita, turekebishe mambo mapema,” alisema na kuongeza:

"Kitendo kile hakiwakilishi matakwa ya wabunge 40 tu wa CHADEMA, wale ni wawakilishi wa mamilioni ya Watanzania, hivyo kinawakilisha kilio cha Watanzania juu ya katiba mpya, tume huru ya uchaguzi...hapa si suala la kumtambua au kutomtambua Kikwete kama inavyopotoshwa."

Bw. Mbowe alisema kuwa umoja wa kitaifa ambao umekuwa ukihubiriwa na watu wengi nchini, utadumishwa kwa nchi kuwa na katiba mpya, ambayo itaondoa sheria mbovu kama ile ya uchaguzi ya mwaka 1985 inayoipatia mamlaka makubwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa urais huku haki ya kupinga matokeo mahali ppote ikiminywa.

Aliongeza kuwa sheria hiyo inayozuia matokeo ya urais kupingwa mahakamani ilifaa zaidi wakati wa chama kimoja ambapo hata mgombea urais alikuwa ni mmoja pia, hivyo hakukuwa na namna au maana yoyote kupinga kuchaguliwa kwake, kwani ilikuwa ama umchague yeye au 'kivuli'.


"Wenzetu Senegal wamekwenda mbali, katika sheria zao, wameunda mahakama ya katiba ambayo ndiyo ina mamlaka ya kumtangaza mshindi wa urais baada ya kuwa imeshasikiliza pande zote katika uchaguzi na imeridhishwa na maamuzi ya tume ya uchaguzi, mahakama ndiyo inatoa final results (uamuzi wa mwisho).

"Afrika Kusini pia wana quite independent commission (tume huru kabisa)...Tanzania hakuna fursa kama hiyo, halafu mshindi wa urais akishatangazwa huna mahali pa kupinga hata kama unao ushahidi...angalia hata Zanzibar, kumetulia na sasa kila mmoja anafurahia kwa sababu walikaa chini wakajadili mambo yao," alisema Bw. Mbowe.

Aliongeza kuwa ni vyema mamlaka husika zikawa sikivu kwa kuangalia umuhimu wa masuala hayo kwa maendeleo ya taifa, badala ya kusubiri mambo yakaharibika ndipo hatua stahili zichukuliwe, akisema kuwa uamuzi wao wa baade utatokana na namna serikali itakavyokuwa imepokea 'ujumbe' wao.

Alisema kuwa inasikitisha kuwa nchi ina viongozi waandamizi ambayo hawawezi au hawataki kutambua muhimu wa nchi kuwa na katiba inayotokana na mchakato unaoukubalika Watanzania wote, bila kujali itikadi mbalimbali walizonazo, akisema kuwa hao ni mbumbumbu wa siasa.

"Watu wanauliza kwa nini siku ile (waliyomsusa Rais Kikwete), ilikuwa ni nafasi nzuri, tulitaka kupeleka kilio chetu, madai yetu katika sauti kubwa inayoweza kusikika kwa uzuri, ulikuwa ni wakati mwafaka, tungeamua kufanya kienyeji tu, sasa hivi kusingekuwa na mjadala wa kitaifa juu ya madai haya.

"Haya ni maslahi ya taifa, si CHADEMA, akina Makamba wanabeza, mbona yeye kawambia wabunge na madiwani wapinge mahakamani, mtu kama Chiligati waziri mwandamizi lakini hajui, hana mamlaka ya kuweka azimio la kutuondoa bungeni, aseme tumevunja sheria ipi ya nchi au kanuni ipi ya bunge, hawa ni mbumbumbu wa siasa,” alisema.

Bw. Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema kuwa inasikitisha kuwa katika vipengele 13 katika hotuba ya Rais Kikwete bungeni, hakugusia suala la umuhimu wa nchi kuwa na katiba mpya au tume huru ya uchaguzi, akisema yamekuwa ni madai ya muda mrefu ya Watanzania wengi.

Akizungumzia hatua ya Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda kutokea katika sherehe za Rais Kikwete kupongezwa, alisema kuwa hayo ni masuala ya mahusiano ya kijamii kati ya mtu na mtu, hayahusiani na msimamo wa mtizamo, kisera na itikadi za chama.

Juu ya suala la baadhi ya viongozi waandamizi wa CHADEMA kusikika wakisema kuwa hawakuunga mkono kitendo cha wabunge kutoka bungeni wakati rais akianza kuhutubia, Bw. Mbowe alisema;

"Huo ni mtizamo mtu binafsi, uamuzi wa chama ulishafikiwa kwa kura na wengi wakashinda...siku zote maamuzi ya vyama ni vikao na katika vikao watu huweza kutofautiana mawazo, hivyo inahitajika maamuzi ya kura." 

7 comments:

  1. Chadema keeps up!,no chance for;Dictatorship style of leadership,&UFISADI-thus everything has the limit,hence enough is enough!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. mbowe kaza uzi, usimsikilize mrema au maalim self, hao tako zamani ni ccm damu na nia yao kubwa si kuwakomboa watanzania bali ni kulilia madaraka, rejea mrema akimkampenia kikwete badala ya mgombea wa chama chake ingawa yeye ni mwenyekiti wa chama hicho NA AKIOMBA APEWE UWAZIRI WA MAMBO YA NDANI, au maalim self yeye ameshapewa umakam na sare ya suti ya ccm, sasa anaona eti kumgomea rais kikwete ni UHAINI!!JAMANI SIASA WEWE MAALIM SELF HATA UNAKUJA DAR UNAFIKIA IKILU HATA BILA KUFIKA BUGURUNI KUONANA NA NDUGU YAKO LIPUMBA!!!UMESAHAU JINSI WANA CUF WALIVOPIGWA RISASI!!
    KATIBA MPYA, TUME HURU YA UCHAGUZI NI LAZIMA,

    ReplyDelete
  3. kaza uzi baba ccm mbumbumbu wanapiga hovyo kelele

    ReplyDelete
  4. Tanzania inahitaji mageuzi ya kimaendeleo, kwa kuangalia vitu vitatu muhimu kama vilivyobainishwa na Mwenyekliti wa CHADEMA, vinginevyo hakuna haja ya kuwa uchaguzi mkuu. Utawala wa udikiteta mamboleo hauna nafasi nchini Tanzania ni bora mambo kuwekwa bayana. Kuna uwezekano wa kuwa na katiba mpya inayokidhi hatua za demokrasia ya kweli na tume huru ili jamii iwe na viongozi inayowataka hata kama hawawezi kuwapa maendeleo wanayotaka lakini ni uchaguzi wao.

    ReplyDelete
  5. Jamani, tuende na mifano lakini tuangalie mbele na nyuma, historia ya tanzania si historia ya nchi nyingine, historia ya zanzibar na utamaduni wa wazanzibari sio sawa na watanganyika. tafiti nyingi zinafanywa kwa kulingania mifano ya tafiti ili utafiti ule unaofanyika upate kusimama na kukubalika, lakini duniani hadi leo hakuna tafiti ilio sahihi na hakiki zote zina kasoro...WITO: kama hakuna maelewano ya kuungana wapinzani katika sera na mikakati yao, sio wote wawe na sera na mkakati wa aina moja , wawe na uniqueness pale pa kumsimamisha mgombea mmoja wa kupinga CCm pafanyike hivyo wasijali wa chadema au wa NCCR, TLP au wengineo na wapige kura ya pamoja kwa mgombea wao.... bila hayo ni kumpigia mbuzi gitaa..hadi CCm ibomoke yenyewe ndani ndio kutakuwa na upinzani au ndani ya ccm watoke watu watakaounda upinzani..

    ReplyDelete
  6. BIG ISSUE NI KATIBA,ULIMWENGU WA KWANZA UMEPITIA YOTE HAYO, HIVYO TUENDANE NA WAKATI ILI AMANI IWE NI YA KWELI, KAMA MAKAMBA NA WENZAKE WANASHIBA KWA NAFASI YA UONGOZI WALIYONAYO WANAPASWA WAFAHAMU KWAMBA KUNA WENGINE WANALALA NJAA HIVYO KWA DHAMANA YA MADARAKA WALIYONAYO WANAPASWA KUWA NA STRATEGY NA WENGINE WASILALE NJAA, PRIOROTY ZIWE KTK SOCIAL SERVICES.

    ReplyDelete
  7. Mkimwona huyo Chiligati mumwambie hizo kauli zake ambazo hazina ufahau wala huwezi kutambua kama ni kiongozi anaongea maneno sijui niseme yamechacha au ni mgando aache kama hana point.

    Ndugu watanzania mkitaka kujua nchi haina raisi utaelewa maneno ya huyu jamaa yeye anaongea kama nani, kama mjumbe wa serikali, wa bunge au ni rais wa tanzania.

    Kama alikuwa na chupa moja mbili kichwani asiwe anaongea kama hana point ya maana. eti atawaondoa bungeni ni rahisi hivyo, aanze kuondoka yeye kwanza. Na nina wasiwasi na uraia wake tumchunguze inawezekana ni mkimbizi.

    Mtanzania kiongozi hawezi kuwa na mawazo mgando namna hiyo. Hatutaki kusikia hizo taarabu zenu tumechoka. Hawa ndio walimpoteza Raisi wetu kikwete akayumba.

    ReplyDelete