Na Tumaini Makene.
KESI inayohusu kashfa maarufu ya ununuzi wa rada ya kijeshi iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka Kampuni ya Vifaa vya Kijeshi ya Uingereza (BAE) itaunguruma mahakamani
nchini Uingereza kwa mara ya kwanza kesho.
Kesi hiyo itafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa muda mrefu uliokuwa ukifanywa na Taasisi ya Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) ambapo kampuni ya BAE ilikiri taarifa zake za hesabu kuhusu rada iliyonunuliwa na Tanzania, hazikuwa sahihi na kuwa, ipo tayari kukiri kosa hilo mahakamani na kulipa kiasi cha Paundi za Uingereza milioni 30 (sh. bilioni 72) kama adhabu na fidia kwa Tanzania.
Taarifa ya kuwa kesi hiyo itafikishwa kesho mahakamani huko Uingereza, inatokana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa hivi karibuni na Ubalozi wa Uingereza nchini, iliyosema kuwa baada ya hatua hiyo ndipo itaweza kutolewa hitimisho juu ya uhusika wa baadhi ya watuhumiwa, kama wana makosa au la.
Taarifa hiyo ya Uingereza iliyotolewa Novemba 10, ikionekana kuwa sawa na kukanusha taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliyotolewa kabla ikimsafisha Bw. Andrew Chenge, mmoja wa watuhumiwa katika kashfa hiyo, iliweka wazi kuwa katika hatua ya uchunguzi iliyokuwa imefikiwa kabla ya kufikishwa mahakamani, hakuna chombo kinachoweza kuhitimisha suala hilo kwa kusema mtu fulani ana makosa au la.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Februari 5 mwaka huu, SFO ilitoa taarifa ya kufikia makubaliano na kampuni ya BAE, baada ya uchunguzi katika mkataba na serikali ya Tanzana.
"Makubaliano hayo, baina ya SFO na BA yalihitimisha shughuli za uchunguzi zilizokuwa zinafanywa na taasisi ya SFO. Hata hivyo, kwa kuwa makubaliano hayo hayajathibitishwa na mahakama si sahihi kwa sasa kusema kuwa uamuzi huo umepitishwa," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa usikilizwaji wa kesi hiyo utaanza kesho na baadaye uamuzi wa kuthibitisha makubaliano hayo utatolewa.
Kabla ya kufikia hatua hiyo ya SFO iliwahi kutoa muda maalumu kwa BAE Systems kukiri makosa yake au kufikishwa mahakamani baada ya kuchunguza na kugundua kuwa mkataba wa ununuzi wa rada hiyo wa mwaka 1999, kati ya Tanzania na kampuni hiyo, uligubikwa na mazingira tata yenye kuashiria wa rushwa.
Kashfa hiyo ya rada, ambayo ndiyo ilisababisha kujiuzulu kwa aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Chenge, iliibuliwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya Uingereza na Tanzania, ambapo ilielezwa kuwa iliuzwa kwa bei ghali isivyo halali, ikidaiwa kuwa bei iliongezwa makusudi, huku kiasi kilichoongezwa kikitumika kama mlungula kuwahonga baadhi ya vigogo wa Tanzania waliokuwa wakihusika kupitisha mkataba wa ununuzi huo.
Tangu kuibuka kwa kashfa hiyo, imekuwa ikidaiwa kuwa 'mchezo' wa kuongeza bei ya rada hiyo kwa kiasi cha sh. bilioni 12, kisha kugawa mlungula huo kwa vigogo ambao ni wanasiasa na watendaji waandamizi serikalini, ilifanywa kwa ustadi mkubwa na dalali (mtu wa katikati) Mtanzania mwenye asili ya Kiasia aitwaye Sailesh Vithlan, ambaye tangu kuibuliwa kwa kashfa hiyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Akiwa wakala, Vithlan alifanikisha ununuzi wa rada hiyo, huku akituhumiwa kuishawishi Tanzania itoe sh. bilioni 16 zaidi ya bei halisi, ambapo inadaiwa tena kuwa alipewa sh. bilioni 12 kama bakishsi ya kufanikisha biashara hiyo. Ni kiasi hiyo alichopewa kama kamisheni ndiyo kilitumika kuwahonga vigogo serikalini.
Mbali ya Bw. Vithlani kuripotiwa kukimbilia nje, akitoroka nchini katika mazingira ya kutatanisha akiwa nje kwa dhamana baada ya kufunguliwa mashtaka, kumekuwepo na ripoti kuwa baadhi ya watu wake wa karibu alioshirikiana nao katika kashfa hiyo, wapo nchini wakitembea huru bila bugudha yoyote. Bw. Vithlani atajwa kuwa katika orodha ya watu wanaosakwa na Polisi wa Kimataifa (Interpol).
Imewahi kuripotiwa mara kadhaa na vyombo vya habari kuwa BAE Systems imekiri kuwapo kwa malipo ya kamisheni kwa dalali wa biashara ya ununuzi wa rada hiyo, ingawa hayakuwekwa bayana, huku msemaji wake, Dick Olver akinukuliwa kusema “Kampuni ya BAE inajutia yaliyotokea na inakubali kubeba mzigo kwa matatizo yaliyotokea.”
Moja ya magazeti maarufu ya Uingereza, ambayo yamekuwa yakifuatilia na kuandika kwa kirefu juu ya kashfa hiyo, The Guardian, lilipata kuripoti kuwa mawaziri wawili wa nchi hiyo, Bi. Claire Short na Robin Cook walijaribu kuzuia 'biashara' hiyo iliyodaiwa kuwa ni ya gharama kwa nchi maskini kama Tanzania, lakini aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Tony Blair alikataa akisema lazima mpango huo ukamilike. Baadaye Waziri Short alijiuzuru ikiwa ni hatua ya kupinga ununuzi huo.
Gazeti hilo liliripoti kuwa hata taasisi kubwa duniani za kifedha na utaalamu wa masuala ya anga kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Masuala ya Usalama wa Anga Duniani (ICAO) ziliwahi kusema kuwa bishara hiyo iliyofanyika mwaka 2001 "haikuwa muhimu na ilikuwa imezidishwa bei".
"Lakini mpango huo uliohusisha Paundi za Uingereza milioni 28 ulianza kuonekana una matatizo pale SFO walipogundua kuwa sehemu kubwa ya bei ya katika mkataba wa ununuzi ilikuwa imeingizwa katika akaunti za benki za siri nje ya nchi, huku ikiaminika kuwa fedha hizo zilitumika kuwahonga wanasiasa wa Tanzania na watendaji wengine serikalini.
"SFO waligundua kuwa pesa hizo ziliingizwa katika benki moja huko Uswisi katika akaunti iliyokuwa ikimilikiwa na Bw. Vithlani...aliyekimbia Tanzania baada ya taasisi ya kuzuia rushwa nchini humo kumshtaki kwa kuwadanganya wachunguzi...mmoja wa wanasiasa wa Tanzania, Bw. Chenge alilazimika kujiuzulu mwaka 2008 baada ya wachunguzi kugundua zaidi ya Paundi za Uingereza 500,000 kwenye akaunti yake huko Jersey. Alikana fedha hizo kutokana na na BAE," liliwahi kuandika The Guardin.
Wakati Bw. Chenge akijiuzulu kutokana na kashfa ya rada baada ya kiasi cha fedha sh. bilioni moja kukutwa katika akaunti yake huo Visiwa vya New Jersey, Uingereza, alivyoviita kuwa ni 'vijisenti' alikuwa ni waziri katika Wizara ya Miundombinu.
Haya tena kaka Chenge mambo ndo hayo hadharani...tutaona mbivu na mbichi.Tutaona kama wewe ni mkweli au msikweli.Tutaona kama wewe ni msafi kadiri ya TAKUKURU au mchafu kadiri ya wapigania 'Uhuru'.Tunasubiri...tutajua.
ReplyDeleteTuwaombe hao waingereza Waturejeshee hiyo change yetu (72 Billion) walau tujenge barabara kilometer kama 80 hivi za lami ili kurahisisha mawasiliano vijijini na mijiji.Hiyo barabara ikikamilika tuipe jina la RADA ROAD
ReplyDeletekama sio RADA ROAD basi CHENGE ROAD.Safi sana kaka...tupo pamoja.
ReplyDelete