07 November 2010

JK aapishwa rasmi.

*Asema sasa kazi ni moja tu, kutekeleza ahadi
*Akiri wapinzani wameipa changamoto CCM
*Kutoa mwelekeo, dira ya Serikali yake Bungeni
*Aagiza vyombo vya usalama kutoruhusu machafuko

Na John Daniel 
JAJI Mkuu wa Tanzania Augustino Ramadhani, amehitimisha mchakato wa uchaguzi kwa kumwapisha rasmi Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake
Dkt. Mohamed Garib Bilal kuongoza nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakati Jaji Ramadhani akimkabidhi Rais Kikwete 'mikoba' ya kuongoza nchi kwa miaka mitano, kiongozi huyo ameanza kwa kuwataka Watanzania kuacha malumbano ya kisiasa na kuungana kujenga Taifa.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Uhuru jana, muda mfupi baada ya kuapishwa, Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa kuanzia sasa kazi yake ni kutekeleza ahadi alizotoa kupitia Ilani ya uchaguzi wa CCM na si vinginevyo.

Alisema licha ya kwamba dira, mwelekeo na mkakati wa Serikali yake, atayaweka wazi bungeni mjini Dodoma wiki ijayo, lakini vyombo vya dola vinapaswa kuwa macho zaidi na kutokubali watu au kundi lolote kuvuruga amani ya nchi kwa kuwa ndilo ngao pekee ya kutoa nafasi kwa Serikali kutekeleza ahadi zake.

"Ndugu zangu uchaguzi umekwisha kazi kubwa iliyobaki ni kutekeleza aahadi na sina shaka na hilo tutayatekeleza kama tulivyofanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Nawashukuru sana wagombea wenzangu sita wa nafasi ya urais, wametuchangamsha kweli katika kampeni wametufanya tuchangamke zaidi, kwa ushindani mliotupa ni lazima chama chetu kigangamane zaidi huko mbele,"alisema Rais Kikwete.

Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu changamoto kubwa inayowakabili yeye viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini ni kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu wa nchi kwa kutibu majeraha yaliyotokana na kampeni za uchaguzi Mkuu.

Alikiri kwamba baadhi ya kauli za wanasiasa zimewachanganya wananchi na kuanza kujenga tabia ya udini, ukabila na ubaguzi wa kimaeneo jambo ambalo lisipofanyiwa kazi kwa haraka linaweza kuleta athari kubwa zaidi kwa Taifa.

"Tanzania inasifika kwa amani na utulivu, tusiharibu sifa hiyo nzuri, viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wa dini, asasi za kiraia na vyombo vya habari tushirikiane kurudisha nchi yetu kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka mitano na tangu tupate uhuru wetu,"alisisitiza Rais Kikwete.

Kuhusu ushindi wake alisema Watanzania wamedhihirisha kwamba bado wana imani na kuipenda CCM, sera zake na yeye mwenyewe na kuwataka wanachama wa chama hicho kutembea kifua mbele kwa kuwa wameaminiwa na kupewa kura za kuongoza nchi.

"Nawashukuru sana Watanzania wote kwa kutuchagua, mmetupa ushindi usio na shaka hata kidogo, kwa ushindi huu wana CCM tembeeni kifua mbele,"alisema.

Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wana CCM walioshiriki kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi, waluiotoa michango yao, mke wake Bi. Salma Kikwete aliyeungana naye katika kampeni pamoja na familia yake.

Alisema katika kampeni zake alihutubia mikutano rasmi za papo kwa papo 706.

Wakati huohuo Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake Bw. Samwel Sitta, alichangamsha hafla hiyo baada ya wananchi kumshangilia kwa nguvu zaidi jina lake ilipotajwa kuwasili uwanjani hapo.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais wa Zimbambwe Robert Mugabe, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Kongo Joseph Kabila, Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma, Rais wa Kenya Mwai Kibaki pamoja na Rais wa Zambia Rupia Banda. 

Pia walikwepo wawakilishi wa Rais wa Uganda, Malawi, Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mabalozi na wageni wengine mashuhuri kutoka nje.

Viongozi wengine wa kitaifa waliokwepo ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, mawaziri wakuu waastafu,wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wengine.

2 comments:

  1. JK utashinda tu hata kwa wizi hilo najua ila ukitaka imani kwa waswahili waziri mkuu mweke Pombe Magufuli na umwache aongoze kama Mkapa alivyoacha akaongoza wizara ya ujenzi. Vinginevyo utakuwa rais ambaye hata ww utakuwa unajua kuwa mm na wengine wengi hatukukubali hata kidogo, kwa kulinda na kutetea uovu ufanywao na rafiki zako.

    ReplyDelete
  2. Mwisho wa wezi wote wa kura zetu unakuja wajiandae kupokea ujira wao.

    mm nasema wewe kikwete hata ukiiba kura za wenye haki lakini fahamu zitakutokea puani pamoja na wachakachuaji wenzako.

    hukumu hapahapa duniani kabla hujafa sibiri kidogo wala si muda mrefu utajionea mwenyewe na hao wezi wenzio.

    ReplyDelete