NAIROBI,Kenya
WAZIRI Mkuu wa Kenya,Bw. Raila Odinga amewatetea mawaziri kutoka ndani ya Chama cha ODM ambao wanatajwa katika kesi za rushwa akisema kwamba
haina maana kwamba tayari wana hatia.
Bw. Odinga aliyasema hayo juzi,wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho lakini akasema kuwa endapo watakutwa na hatia watakumbana na mkono wa sheria na akayafananisha madai na shutuma hizo za sasa kama matukio ya mwizi anayefukuzwa mitaani kabla ya kukumatwa na kufunguliwa mashtaka.
Waziri Mkuu huyo alisema, itakuwa ni makosa kumshutumu Waziri wa Maji,Bi. Charity Ngilu kutarajia eneo la Ukambani kupata maji sawa na kama yalivyo maeneo ya Kiambu, Kericho, Kisii na Kakamega ambayo yanapata mvua ya kutosha.
Lakini akasema kuwa chama hicho kitatoa msaada mkubwa katika vita dhidi ya rushwa,wahujumu uchumi na umasikini.
Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu aliwaeleza wapinzani kisiasa kujiandaa na mapambano kisiasa katika uchaguzi ujao wa mwaka 2012.
Bw. Odinga,ambaye ndiye kiongozi wa Chama cha ODM,alisema kuwa chama chao bado kina nguvu hususani katika eneo la Rift Valley na akasema kuwa kimejichimbia mizizi katikati mwa jimbo hilo "ODM bado ni chama cha kushinda mwaka 2012," alisema Bw. Odinga.
Hata hivyo baadhi ya wabunge kutoka maeneo ya Kalenjin ambao ni washirika Makamu wa kiongozi huyo wa ODM,Bw. William Ruto,ambaye kwa sasa yupo nchini Uholanzi kukutana na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia Makosa ya Uhalifu wa Kivita ICC,Bw. Luis Moreno-Ocampo hawakuhudhuria.
Wabunge hao wanadai kuwa wataikacha ODM,lakini hata hivyo Waziri Mkuu huyo alisema kuwa Bw.Ruto bado ni mwanachama wa ODM na bado hajakiandikia chama barua ya kujing'atua.
Alisema kuwa vikao vya sasa vilivyofanyika katika maeneo ya Kipkelion, Kericho na Nandi ambazo ni ngome kuu za Bw.Ruto vimeonesha kuwa Chama hicho cha ODM ni maarufu katika maeneo hayo.
Baadhi ya wabunge walipokuwepo katika mkutano huo kutoka kabila la Kalenjin ni pamoja na Profesa Margaret Kamar, Bi.Joyce Laboso, Bw.Musa Sirma, Bi. Beatrice Kones, Bw. Julius Murgor na Bw. Henry Kosgey.
Bw.Odinga alitangaza kuwa chama chake kitafanya uchaguzi wa ngazi ya chini mwezi Desemba mwaka huu na uchaguzi ngazi ya taifa mapema mwaka ujao.
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali ya kitaifa imefanya vizuri ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita lakini ukosefu wa ajira, kupunguza umaskini na usawa bado ni tatizo kubwa.
No comments:
Post a Comment