21 November 2010

Jinsi ya kumdhibiti mpenzi anayepiga 'mizinga' .

Na Shangazi Glady

NI Jumapili nyingine nipo nanyi wasomaji wa safu hii kwa ajili ya kuendelea kuelimisha mambo mbalimbali yanayohusu mahaba.Leo nitazungumzia kuhusu  tabia za baadhi ya watu walio katika uhusiano ya
mapenzi kuwa na tabia ya kupenda kuwapiga mizinga wenzai (kuomba fedha).

Tabia hii ipo zaidi kwa upande wa wanawake, ingawa siku hizi hata wanaume nao wameingia katika mkumbo huu.

Si ajabu kumsikia mwingine akisema; "Mimi nina kibuzi changu bwana, kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nitakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri, maisha yanaendelea. Yaani ni full kujiachia."

Si hivyo tu, wapo wanaume ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wana uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.

    Unaweza kumsikia mwanaume akisema; "Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananipa anajua akinizengua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia. Yule ndiyo mwanamke wa kuwa naye bwana."

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kupitilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida  akaomba msaada umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mwambie  huna,kisha mwangalie ni kwa jinsi gani mnaweza kusaidiana kutatua tatizo linalomkabili.

Itakuwa sio busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta mtu anachuna mwenzake ili apate fedha za starehe.

Mfano leo hii umeomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri unataka akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe out bila kujali kama ana fedha au hana. Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka?

Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu nani? Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila wakati tena kwa ajili ya matumizi e ambayo si ya msingi, zingatia mambo yafuatayo.

MWAMBIE UKWELI

Kama huna pesa mwambie ukweli mpenzi wako, usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza.

Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki au kile. Mwanaume hatakiwi afahamike siku ambayo ana pesa au ambayo hana.

Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi stahili za kutembea.  Mwanamke akijua hilo naye ataongeza mizinga, kuwa makini.

Kuwa mkweli siku zote, utakapokuwa mkweli kwake atakuheshimu. Siku hazilingane, uwe una fedha au huna asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa katika maisha.

         JENGA MAZINGIRA YA YEYE KUKUSAIDIA

Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

BANA MATUMIZI

Kuna wanaume wengine tangu wanapowataka wasichana wanakuwa wafujaji. Wanatumia nguvu ya fedha kuwapata wasichana.
Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli  ni kwamba unakuwa hauna uwezo kama unaoonesha.

Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa unazo.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi, hivyo epukana na tabia hiyo.

No comments:

Post a Comment