21 November 2010

Jimbo Kuu Katoliki Mbinga na mkakati wa kutokomeza malaria.

*Wajerumani wajenga kituo cha kutoa elimu
*Kasi ya maambukizi ya ugonjwa yapungua
*Hospitali ya Lituhi yaomba wataalamu


Na Kassian Nyandindi
UGONJWA wa malaria ni ugonjwa tishio kwa maisha ya wananchi wengi duniani. Tatizo hili ni kubwa kwa familia maskini kuliko kundi lingine la watu.
Madhara ya malaria nmdiyo yanachochea jitihada tunazoziona za kutokomeza ugonjwa huo katika sehemu mbalimbali duniani.

Jitihada za kuendelea kupambana na malaria bado zinahitajika zaidi ili kuwa na jamii yenye afya bora.

Ni ugonjwa wa malaria unaenezwa  na mbu wenye vimelea vya malaria.

Hapa  Tanzania ugonjwa wa malaria ni tishio kwa maisha ya wananchi, hasa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano.

Ingawa jitihada za kupambana na ugonjwa huo zimekuwa zikiendelea bado kuna changamoto kubwa. Kwa sasa takwimu zinaonesha kuwa watu zaidi ya milioni 20 inakadiriwa kwenda  hospitali kutibiwa kila mwaka hugundulika kuwa na vijidudu vya ugonjwa huo, ambapo kati ya hao 60,000 hufariki dunia wengi wao wakiwa watoto chini ya umri huo.

Katika nchi za Afrika Mashariki inakadiriwa kuwepo wagonjwa milioni 60. Takwimu hizo zinaonesha kuwa watu 1,000,000 huripotiwa kufa kila mwaka.

Watu 291 huripotiwa kufa kila siku kutokana na ugonjwa huo, wengi wao wakiwa watoto wadogo. Takwimu hizo zinaonesha kuwa  kila baada ya saa moja watu wanaokufa kwa ugonjwa huo ni zaidi ya kumi.

Idadi hii ni kubwa hasa kwa kuzingatia kuwa tiba na kinga ya ugonjwa huo ipo, lakini bado idadi ya vifo inaongezeka kila kukicha na kutishia uhai wa wananchi wengi.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya Katibu wa Afya Jimbo Kuu Katoliki la Mbinga Mkoa wa Ruvuma Padri Raphael Ndunguru, anasema katika kupambana na ugonjwa wa malaria, jimbo hilo kwa kushirikiana na shirika la habari la Televisheni (RTL – 2) lililopo  Ujerumani linajenga kituo cha kupambana na malaria.

Ujenzi wa kituo hicho unafanyika katika kijiji cha Lituhi Wilaya mpya ya Nyasa Ruvuma.

Anasema mwaka 2008 wageni kutoka Ujerumani walitembelea hospitali ya Lituhi hususani mwambao mwa Ziwa Nyasa, ambapo waliweza kuona jinsi  watu wanavyokabiliwa na tatizo la ugonjwa huo.

Anasema waliporudi Ujerumani walishawishi  shirika hilo la habari kufanya kampeni ya kuchangisha fedha kutoka kwa raia wenye mapenzi mema kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria katika mwambao wa Ziwa Nyasa ili ziweze kufanya shughuli za ujenzi wa kituo cha kupambana na ugonjwa huo katika kijiji hicho cha Lituhi.

 Padri Ndunguru anaeleza kuwa wakati kampeni hiyo inafanyika huko, kulikuwa na mwitikio mkubwa kutokana na uhamasishaji uliofanywa na kwamba fedha zilizopatikana ziliwasilishwa kwenye shirika linalosimamia ujenzi wa mradi huo wa malaria liitwalo “Action Medeor” la nchini Ujerumani.

Anabainisha kuwa ujenzi wa mradi huo wasimamizi wakuu ni shirika hilo, ambapo pia wanafanya shughuli ya kukarabati kituo cha afya Lundu, Nangombo Mango na Makwai Wilayani Nyasa ikiwemo na usambazaji wa vyandarua vilivyowekwa dawa inayodumu kwa muda mrefu ambavyo vinauzwa kwa gharama nafuu kwa wananchi na kugawiwa bure kwa wanavikundi vya ngoma vinavyo hamasisha  kupambana ya malaria.

Mradi huo unatoa elimu kwa jamii namna ya  kujikinga na ugonjwa huo, uuzaji wa vyandarua kwa bei nafuu na kuwawezesha wahudumu wa afya kuwapatia vyombo vya usafiri, yaani baiskeli moja kwa kila kijiji ili waweze kuratibu wajibu wao ipasavyo.

Jumla ya baiskeli 50 aina ya phoenex zenye thamani ya sh. milioni sita zimegawiwa kwa wahudumu wa afya waliopewa mafunzo ya jinsi ya kuielimisha jamii jinsi ya kupambana na ugonjwa huo katika mwambao wa Ziwa Nyasa katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na Jimbo kuu Katoliki la Mbinga.

 Katibu huyo wa afya wa jimbo hilo anasema mradi huo wa malaria unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, hivyo ulianza rasmi   mwaka 2008 utamalizika  mwaka 2012.

Anasema gharama za ujenzi wa mradi huo zitatolewa na mfadhili  mara baada ya kukamilika kwa ujenzi.

"Uzinduzi wa ujenzi wa kituo kikuu cha mradi wa malaria unaoendelea kujengwa Lituhi ulizinduliwa Oktoba 4, mwaka 2009 na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Dkt. Aisha kigoda," anasema na kuongeza;

“Tangu  mradi huu uanzishwe wagonjwa wengi wa malaria katika mwambao mwa Ziwa Nyasa wanaofika katika vituo vyetu vya afya kwa ajili ya matibabu tunawaelimisha jinsi ya kupambana na ugonjwa huo."

“Kutokana na elimu tunayoendelea kuitoa katika jamii, wagonjwa wa malaria wengi wanafika mapema kutibiwa baada ya kuona tu dalili za awali na uelewa sasa umekuwa mkubwa tofauti na miaka ya nyuma vifo vilikuwa vikijitokeza kwa wingi kutokana na watu kuchelewa kupatiwa matibabu”, anasema Padri Nduguru.

Anaongeza kuwa idadi ya wagonjwa wa malaria mwambao mwa ziwa hilo inapungua kila siku kutokana na wananchi kupata elimu elimu ya kupambana na malaria.

Anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni hospitali ya Lituhi kuwa haina watumishi wa kutosha. Anasema wanaiomba serikali isaidie kutatua tatizo la uhaba wa watumishi ili kuongeza ufanisi wa kutoa huduma.

Binafsi nasema malaria husababisha upotevu wa nguvu kazi ya Taifa letu ukizingatia kuwa inaathiri watoto wadogo. Kutokana na madhara ya malaria kila Mtanzania ana jukumu la kupambana na ugonjwa huo.




 

No comments:

Post a Comment