04 November 2010

CCM yaubeba mkoa wa Kagera.

Na Livinus Feruzi, Bukoba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi katika majimbo manne mkoani Kagera, yakiwemo mawili ya Wilaya ya Karagwe na moja la Bukoba vijijini, na
kufanya majimbo ambayo yamekwisha
tangazwa kuchukuliwa na CCM mkoani Kagera kufikia saba.

Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Wchaguzi wilayani Karagwe, Bw. Ernest Mwinga alisema kuwa katika jimbo la Kyerwa, mgombea wa CCM, Bw. Eustace Katagira ameshinda kwa
kupata kura 40, 260.

Bw. Katagira amefuatiwa na Bw. Kato Innocent wa CHADEMA aliyepata kura 22,499 na Bw. Merchoir Bulaine wa TLP amepata kura 672.

Katika jimbo la Karagwe, Bw. Mwinga alimtangaza aliyekuwa akitetea kiti hicho, Bw. Gosbert Blandes wa CCM kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kupata kura 36,065 akifuatiwa na Bw. Deusdedith Kahangwa wa kupitia CHADEMA aliyepata kura 29,711, Bw. Peterson Mushenyerwa wa NCCR-Mageuzi aliyepata
kura 368 na Madanio Swalehe wa CUF aliyepata 263.

Kwa upande wa madiwani, kata 18 zimechukuliwa na CCM na CHADEMA imepata ushindi katika kata tano.

Wakati huo huo Msimamizi wa Jimbo la Bukoba Vijijini, Bi. Beatrice Dominick alimtangaza Bw. Jasson Rweikiza wa CCM kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kupata kura 57,852, akifuatiwa na Bw. Alistides Ndibalema wa CHADEMA aliyepata kura 5,859.

Mgombea mwingine alikuwa Bw. Twaha Taslima wa CUF aliyepata kura 4,565. Kwa upande wa udiwani CCM imepata kata 29 na CUF ilipata kata moja.

Katika jimbo la Ngara, Bw. Deogratias Ntukamazina wa CCM ametangazwa kuwa mbunge katika jimbo hilo kwa kupata kura 37,502.

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Bw. Mathias Ezekiel Mwangu alisema kuwa Bw. Ntukamazina alifuatiwa na Luhuza Samwel Mugisha wa NCCR Mageuzi
aliyepata kura 18,261 na Robert Robinson Musilla wa CHADEMA aliyepata kura 1,962.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo kata zote 20 za jimbo hilo zimechukuliwa na CCM, ambapo watu waliojiandikisha katika jimbo hilo ni 128,226, waliopiga kura 61,051, kura
zilizoharibika ni 3,326, kura halali ni 57,725.

Majimbo mengine yaliyotangazwa kuchukuliwa na CCM ni Bukoba mjini, ambalo lilichuliwa na Balozi Khamis Kagasheki na Chato ni Dkt. John Magufuli, Muleba Kaskazini aliyeshinda ni Bw. Charles Mwijage, Muleba Kusini ni Profesa Anna Tibaijuka.

Jimbo pekee la Biharamulo limechukuliwa na upinzani, ambapo Dkt. Anthony Gervas Mbassa wa CHADEMA ameibuka kidedea. Jimbo la Nkenge uchaguzi wa mbunge uliahirishwa kutokana na kutofika kwa karatasi za kupigia kura. 

No comments:

Post a Comment