29 October 2010

Wenger amwagia sifa Walcott.

LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amempongeza mchezaji wake, Theo Walcott kwa jinsi anavyokuwa na uchu anapokaribia langoni mwa adui, baada ya juzi kuifungia timu yake mabao dhidi ya Newcastle, yaliyoifanya timu hiyo isonge mbele katika michuano ya Kombe la Ligi.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England, amerejea uwanjani baada ya kukaa nje kwa muda na kufunga mabao mawili kwa kila nafasi aliyopewa na mlinda mlango wa Newcastle, Tim Krul katika
ushindi mnono wa mabao 4-0, iliyoibuka nayo Arsenal katika mechi hiyo ya juzi.

Katika mchezo huo, Krul alianza kwa kujifunga mwenyewe kabla ya Nicklas Bendtner, kupachika bao la pili na  Walcott akapachika mabao hayo mawili yaliyoisukuma timu hiyo kwenye hatua ya robo fainali.

Kutokana na mchango huo, Wenger alimpongeza sana mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 21 akisema mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya Watford, ambaye alipachika bao la tano msimu huu ameanza kurejea kweenye kiwango chake.

"Walcott msimu huu amekuwa na uchu mbele ya lango," Wenger aliiambia  Sky Sports. "Kugusa kwake mara ya kwanza uwanjani kumekuwa bora, ni kijana mwenye akili na kwa sababu hiyo, ataendelea kuboreka," aliongeza Wenger kabla ya kusema kuwa alitoweka mwanazoni mwa msimu na sasa amerejea tena, baada ya kupona majeraha.

Mbali na Walcott, vilevile Bendtner naye alifurahi kufunga goli baada ya kuwa fiti tena na kocha Wenger, anajivunia wachezaji hao wawili kucheza vyema na kuleta ushindani katika mechi hiyo, iliyofanyika kwenye Uwanja wa St James' Park.

Alisema: "Mara zote kocha huwa akifurahi kwa washambuliaji wanapofunga mabao. Wameweza kumaliza mechi bila kuumia na kwa sasa kiafya wapo fiti, wameweza kuleta mapinduzi baada ya kupona."

No comments:

Post a Comment