LONDON, England
TIMU ya Newcastle United, imetoa taarifa ikisema kwamba inajiandaa kufanya mazungumzo na kocha wake, Chris Hughton. Magpies imelazimika kutoa taarifa hiyo, kutokana na
kuwepo kwa tetesi za kwamba Hughton, anajiandaa kuitema klabu hiyo.
Vyombo vya habari, pia vimekuwa vikieleza kuwa klabu hiyo inahana kutafuta kocha mwingine na fedha za kumuajiri, baada ya kuondoka Hughton.
Hata hivyo, jana klabu hiyo ya Kaskazini Mashariki mwa England, ilisema itafanya mazungumzo na Hughton, kuhusu mkataba mpya wakati mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Katika taarifa klabu hiyo ilieleza: "Chris ni kocha wetu na ataendelea kuwa kocha wetu, hivyo ndivyo ilivyo.
"Ni jukumu letu kufanya mazungumzo naye tena kuhusu mkataba wake mwisho wa mwaka," aliongeza.
Taarifa hiyo imekuja wakati Newcastle, ikitupwa kirahisi nje ya michuano ya Kombe la Ligi (Carling Cup), baada ya kufungwa na Arsenal mabao 4-0 katika mechi iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa St James' Park.
Matoke hayo pia yanadaiwa kuiweka njia panda hatima ya kocha huyo, baada ya kumalizika mechi hiyo.
Akizungumza na Sky Sports alisema: "Itakuwa ni vigumu kutoathirika, wote tunafahamu kilichotokea kwenye televisheni na kilichooneshwa kwenye televisheni, lakini siwezi kufanya kitu chochote kuhusu jambo hilo, nitajitahidi kufanya kila niliwezalo kwenye kazi yangu.
"Msimu uliopita nilikuwa na jukumu la kuhakikisha naipandisha Ligi Kuu timu hii na nikaweza kufanya hivyo na msimu huu, nina kibarua cha kuhakikisha naibakiza Ligi Kuu timu hii na bado tupo karibu na mpango huo na tunafanya vizuri," aliongeza.
No comments:
Post a Comment