29 October 2010

Watanzania wanataka rais wa 'hapa hapa'.

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa sasa Watanzania wanahitaji Rais wa 'hapahapa' na sio Rais 'kiguu na njia'.
Profesa Lipumba alisema kuwa wananchi wanataka serikali ambayo haina matumizi ya anasa zikiwemo safari zisizo za lazima za nje ya nchi.

"Wananchi hawamtaki Rais ambaye anaona kwenda New York ni sawa na kwenda Chalinze," alisema Profesa Lipumba jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya kuelimisha mpiga kura iliyoandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF).

Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF na anagombea nafasi ya urais kupitia chama hicho kwa mara ya nne, alisema katika kampeni zake za nchi nzima amegundua kuwa wananchi wanaumia kwa maisha duni.

Alisema licha ya wananchi kuahidiwa maisha bora, lakini hali imekuwa tofauti na kipimo chao kikubwa ni bei ya sukari ambayo 2005 ilikuwa kati ya sh. 500 na 600 lakini sasa ni kati ya sh. 1,700 na 2,000 sehemu nyingi.

Alieleza ahadi za ajira kuwa zilikuwa milioni 1, lakini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinadai kuwa kimevuka malengo, lakini hazionekani na badala yake vijana wengi wameingia katika kuuza karanga, maji na kuokota chupa za maji zilizotumika.

Profesa Lipumba pia alitoa kasoro kadhaa katika sekta za elimu, umeme, maji, afya huku akieleza kuwa watoto wa masikini wanalazimika kusoma katika shule ambazo hazina walimu, maabara wala maktaba.

Alieleza kuwa chama chake kikiingia madarakani kitajali wazee, walemavu na kuhakikisha kwamba kodi zinalipwa ikiwemo migodi ya dhahabu ili fedha zinazopatikana zitoe huduma kwa wananchi.

Washiriki wa semina hiyo wakichangia katika mada ya "Watanzania na uchaguzi 2010" iliyotolewa na Omary Kassera wa Dar es Salaam walieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo inayostahili kutoa elimu kwa wapiga kura.

Lakini, baadhi ya washiriki walidai kuwa NEC haitaki kuifanya kazi hiyo kwani wako ambao ndiyo wamewateua wanafaidika na ujinga wa wapiga kura.

"Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni lazima ivunjwe na iwepo tume huru," alidai mshiriki mmoja.

No comments:

Post a Comment