*Kuzungumza na waandishi wa habari kesho.
Na Grace Michael
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupititia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwaogopa
wapinzani na kutowachagua kwa kuwa wamekata tamaa na kugeuka majuha wa matusi badala ya kushindana kwa sera.
Rais Kikwete alisema hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika katika Jimbo la Segerea Kata ya Kiwalani na Jimbo la Ukonga katika Kata ya Kivule.
"Jamani wananchi ogopeni sana watu waliokata tamaa, ni hatari kwa nchi na kuwaadhibu ni kuwanyima kura siku ya Jumapili, wamegeuka kuwa magenge ya watukanaji, vinywa vyao havitamaniki sijawahi kuona. Mikutano yao yote ni kutukana, hata jana (juzi) nilipata taarifa zao za kutukana...CCM kamwe haiwezi kufanya hivyo kwa kuwa inatambua umuhimu wa amani na utulivu," alisema Dkt. Kikwete.
Aliwaomba wananchi hao kuichagua CCM kwa kuwa ndiyo bora kwa mipango, sera na utekelezaji wa ilani zake na imeiongoza vizuri nchi hii na sasa maendeleo yaliyopo yanaonekana kwa macho katika sekta zote na hayawezi kulinganishwa na miaka iliyopita.
"Sera za CCM ndizo nguzo na hatuchochei chuki miongoni mwa jamii kama wenzetu wanavyofanya kwa kueneza udini, ukabila. CCM hatubagui mtu yoyote kwa rangi, udini wala kabila na wala vyama wanavyotoka hivyo chagueni CCM ili iweze kusimamia amani na utulivu wa nchi hii," alisema Rais Kikwete.
Mbali na kueleza hayo pia alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea Dkt. Makongoro Mahanga na kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Jimbo la Ukonga ambalo kwa sasa limegawanywa na kupatikana jimbo jipya la Segerea.
Akizungumzia sekta ya elimu alisema kuwa pamoja na juhudi kubwa iliyofanyika katika sekta hiyo, lakini bado mambo mbalimbali yanafanywa ili kuhakikisha sekta hiyo inajitosheleza kwa kuwa na walimu wenye uwezo, maabara, vifaa vya kufundishia na ifikapo mwakani kila mtoto atakuwa na uhakika wa kuwa na kitabu.
"Wapo wanaosema JK anasafiri sana, lakini bila ya baba kutoka nje kutafuta watoto hawawezi kupata chakula na kutembea kwangu kumezaa matunda mazuri yakiwemo ya kuchapishiwa vitabu na wenzetu wa Marekani na mambo mengine mengi mazuri ambayo yana faida kubwa kwa wananchi wetu," alisema.
Alisema kuwa ili elimu iendelee kuboreka, ni lazima iwe kipaumbele cha serikali kwa kutenga fedha nyingi zitakazosaidia sekta hiyo kwa kuwa hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na elimu bora.
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema kuwa vituo vya afya katika jimbo la Segerea vitapandishwa hadhi ili viwe hospitali ndogo na vikidhi mahitaji ya wananchi wa eneo husika lakini pia watahakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Akizungumzia ugonjwa wa UKIMWI aliwataka wananchi kufuata maelekezo ya viongozi wa dini ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuwa hauambukizi kwa bahati mbaya.
"Hili nalazimika kulisema kwa kuwa Dar es Salaam maambukizi yako juu, tunahudumia wagonjwa zaidi ya elfu sitini na tunaahidi kuendelea kulihudumia kundi hili lakini UKIMWI unaweza ukauepuka kwa kufuata maneno ya viongozi wa dini," alisema.
Pia lizungumzia tatizo la maji ambalo alisema kuwa juhudi zinazofanywa kwa sasa zitalifanya tatizo hilo kuwa historia kwa kuwa vyanzo mbalimbali vya maji ikiwemo Kimbiji, Mpera, Ruvu Chini na Ruvu Juu vinaendelea kufanyiwa maboresho makubwa lakini pia kujengwa visina 20 katika maeneo ya Kimbiji na Mpera.
Akizungumzia tatizo la msongamano uliopo jijini Dar es Salaam alisema kuwa CCM imeweka kipaumbele katika kuboresha barabara mbalimbali za ndani ili ziweze kupunguza msongamano lakini pia kuna mipango au miradi ya mabasi yaendayo kwa kasi pamoja na ujenzi wa barabara za juu.
"Huu msongamano tutaukabiri tu, tutatumia hata reli ya kati kwa muda ambao itakuwa haina kazi, lakini tunaboresha barabara za ndani ili magari mengine yaweze kutumia barabara hizo na kupunguza msongamano kwa barabara kubwa," alisema Rais Kikwete.
Ahadi kubwa aliyoitoa kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga, ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mambasa, Kivule hadi Msongola ambapo alisema kuwa fedha kwa ajili ya barabara hiyo zipo na kinachosubiriwa ni kulipwa fidia kwa wenye vibanda ili wapishe ujenzi huo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete anatarajiwa kuwa na mahojiano na vyombo vya habari, maswali yataulizwa na kujibiwa papo kwa papo, yatarushwa moja kwa moja kesho kuanzia saa mbili usiku.
No comments:
Post a Comment