Na Tumaini Makene
PAMOJA na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuendelea vizuri baada ya mgogoro wa uchumi duniani, serikali mpya baada ya uchaguzi ujao inakabiliwa na changamoto
kubwa ya kuhakikisha kuwa matumizi ya serikali yanaendana na mapato ya ndani ya nchi.
Imeelezwa zaidi changamoto hiyo itasababishwa na mahitaji mengi ya kisera ambayo kimsingi ni matumizi ya serikali kwa mfano kuajiri walimu wapya, wauguzi na madaktari katika sekta ya afya, kulipa mishahara ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali, pamoja na kuchangia katika miradi mingine ya maendeleo kama ujenzi wa barabara.
Imefafanuliwa kuwa tofauti hiyo ya serikali kutumia kiasi kikubwa katika matumizi yake kuliko inavyokusanya kutoka katika vyanzo vyake vya ndani ya nchi inapaswa kurudia hali nzuri kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2007 na 2008, ambapo, utegemezi wa serikali katika kujiendesha ulikuwa imepungua na kufikia rekodi nzuri.
Hayo yalisemwa jana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bw. John Wakeman-Linn, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha ripoti juu ya hali ya uchumi kwa nchi maskini zilizoko Kusini mwa Jangwa la Shahara, Tanzania ikiwa ni mojawapo.
Akifafanua juu ya dondoo za ripoti hiyo, alizozitoa katika wasilisho lake mbele ya wadau mbalimbali wa masuala ya uchumi na waandishi wa habari, Bw. Wakeman- Linn alisema “pamoja na kuwa Tanzania iko katika mwelekeo sahihi, wenye matumaini, bado serikali mpya itakabiliwa na changamoto kubwa hasa katika kuhakikisha inapunguza tofauti kubwa ya matumizi ya serikali na kipato hasa kinachotokana na mapato ya ndani.
“Changamoto za kisera katika matumizi ya serikali zitakazokuwepo ni kama vile katika uendeshaji wa serikali kama vile kulipa mishahara, kuajiri walimu, madaktari…kushiriki kuchangia miradi mingine kama vile miundombinu ya barabara n.k…unajua kwa namna moja ama nyingine utekelezaji wa changamoto hizi unaongeza gharama za serikali,†alisema Bw. Wakeman-Linn na kuongeza;
“Sasa matumizi ya serikali yanapaswa kuendana na mapato ya ndani ya nchi, pale mapato ya ndani ya nchi yanapokuwa yako chini, hayaendani na matumizi ya serikali ambayo yako juu ni tatizo…hivyo lazima mapato ya ndani yatosheleze kuendesha matumizi ya serikali…swali la msingi linapaswa kuwa ni vipi mapato hayo yataweza kuongezwa au kuongezeka.â€
Dondoo za wasilisho la Bw. Wakeman-Linn unaonesha kuwa matumizi ya Serikali ya Tanzania ni makubwa kuliko inavyoweza kukusanya mapato yake ya ndani ambayo kwa hakika ndiyo yanapaswa kuendesha serikali.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa tofauti ya mapato na matumizi haikuwa kubwa katika miaka ya 2003 hadi 2006, lakini ikaanza kupanda mwaka 2006 hadi sasa.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, aliyekaribishwa kufungua kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ya IMF, alisema kuwa ripoti za namna hiyo ni changamoto kwa ajili ya kujua tunakotoka, tulipo na tunakokwenda.
Prof. Ndulu alisema kuwa ni muhimu kuwa na ripoti kama hiyo ya IMF kwani zinasaidia katika upangaji na utekelezaji wa sera mbalimbali.
“Ni ripoti nzuri inaonesha namna gani nchi za Afrika zimeweza kuhimili kuongezeka kwa bei ya chakula, mafuta na kuyumba kwa uchumi…inaonesha kuwa tumeweza kukua kwa uzuri, huko tunakokwenda kufufuka na kuboreka kwa uchumi wa Afrika kutaendelea.
“Inaonesha kuwa tumekua kwa asilimia 2.2, kukiwa na matarajio ya kufikia asilimia 5, mwaka 2011 tunaweza kufikia asilimia 6, huku wenzetu wakubwa watakuwa wanakua polepole isipokuwa China. Kwa upande wa Tanzania ripoti inaonesha kuwa tumehimili vizuri, hali yetu ya uchumi ni asilimia 6-7 kwa mwaka,†alisema Prof. Ndulu na kuongeza;
“Hali ya akiba yetu ya fedha za kigeni ni nzuri, asilimia ya deni letu la nje ni asilimia 30 ya pato letu, wakati wapo wenzetu wana asilimia kubwa sana…lakini kwa kipindi hiki tunapaswa kujinusuru na ongezeko la matumizi ya serikali, pengo la matumizi na mapato lipungue, yaendane sawa.â€
Prof. Ndulu alisema kuwa kutokana na nchi nyingi zinazoendelea kuonesha hali nzuri ya ukuaji wa uchumi, baada ya mgogoro wa uchumi duniani kuliko nchi zilizoendelea, wawekezaji sasa wanafuata kule ambako uchumi unaonesha matumaini ya kwenda vizuri.
“Wawekezaji sasa wameanza tena kuiangalia Tanzania, sasa wakati tunazipokea fursa hizo za wawekezaji, ni vyema uwekezaji huo uwe wa manufaa kwa Tanzana kwanza,†alisema Prof. Ndulu.
Ripoti hiyo ya IMF imekuja siku chache baada ya utafiti wa Asasi ya Twaweza kuonesha kuwa katika kila shilingi moja inayokusanywa na serikali kwa mapato ya ndani, matumizi ni sh. 1.9, ambapo ilielezwa kuwa pengo kati ya kinachokusanywa na kinachotumiwa huzibwa kwa njia ya kukopa na kwa njia ya kupokea misaada ya kibajeti ya nje, hali ambayo si nzuri kiuchumi.
No comments:
Post a Comment