01 November 2010

Twiga Stars yaanza vibaya Afrika Kusini.

Na Zahoro Mlanzi, Mashirika ya habari

TIMU ya Wanawake ya Taifa 'Twiga Stars', jana ilianza vibaya kampeni zake za kutwaa ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake  baada ya kufungwa mabao 2-1 na
wenyeji Afrika Kusini 'Banyana banyana' katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sinaba nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ilieleza kwamba wenyeji walicheza vizuri katika mchezo huo wa ufunguzi huku wakishangiliwa na maelfu ya mashabiki wao waliokuwepo uwanjani hapo.

Banyana Banyana walifunga bao la kwanza dakika ya 35 lililofungwa na mshambuliaji wao, Mamphasha Popela aliowafanya mashabiki wa timu hiyo kuripuka kwa shangwe na nderemo uwanjani hapo.

Lakini furaha hiyo iliingia dosari baada ya kiungo mshambuliaji wa Twiga Stars, Esther Chabruma kusawazisha bao hilo dakika ya 43 na kufanya timu hizo kwenda
mapumziko zikiwa sare.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Banyana Banyana kufunga bao la pili dakika ya 86 lililofungwa na kiungo Makhabane Mamello na kufanya mashabiki kushangilia upya kwa nguvu.

Akizungumza kwa simu kutoka huko, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Mkwassa alisema waamuzi wa mchezo huo waliwabeba wenyeji kwani bao la pili lililofungwa kwa mkwaju wa penalti haikuwa halali.

"Mchezo umemalizika hivi karibuni kwa kufungwa mabao 2-1 lakini kiukweli wachezaji wangu walicheza vizuri ila mwamuzi aliwapa bao la pili kwakuwa sijui ni wenyeji kwani mazingira ya penalti yalikuwa na utata," alilalamika Mkwassa.

No comments:

Post a Comment