Na Zahoro Mlanzi
MAELFU ya wadau wa soka nchini, wanatarajia kwenda kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Kocha wa viungo na mshauri wa saikolojia wa timu ya
Simba, Syllersaid Mziray 'Super Coach' leo kwenye viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam.
Mziray alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi katika hospitali ya Agakhan jijini baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari hizi, jana mchana alifika nyumbani kwa kocha huyo Tabata Magengeni na kukutana na umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki waliofika nyumbani hapo kutoa pole kwa familia ya kocha huyo.
Baadhi ya watu waliofika kutoa pole ni pamoja Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Juliana Yasoda ambaye alionekana kila wakati kujadiliana jambo na kaka wa marehemu (jina halikufahamika mara moja).
Mbali na kiongozi huyo, baadhi ya wachezaji wa Simba, kipa Juma Kaseja, Emmanuel Okwi na Joseph Owino waliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' kutoa pole kwa wafiwa.
Akizungumza mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini kwani si msemaji wa familia, aliliambia gazeti hili kwamba Mziray atazikwa leo saa 10 jioni kwenye makabuli ya Kinondoni, Dar es Salaam.
"Tunatarajia kuzika kesho jioni (leo) kule Kinondoni na saa tatu asubuhi wanafamilia wote watamuaga hapa nyumbani na wadau wa michezo, wafanyakazi na watu wengine hao watamuaga kuanzia saa sita mchana mpaka saa tisa katika viwanja vya Biafra," alisema ndugu huyo wa marehemu.
Mziray alizaliwa Novemba 11, 1957 na kupata elimu ya msingi katika shule tofauti tofauti ambazo ni Ifunda, Low Academic (Iringa), Mpechi (Njombe), Songwe (Mbeya), Butimba (Mwanza), Lukajunge (Karagwe) na kumalizia Wami (Morogoro).
Elimu ya sekondari aliipatia katika shule za Malangali (Iringa) na Milambo iliyopo Tabora na baadaye kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mwaka 1981 alikwenda kusoma Bulgaria ambapo alipata Shahada ya Pili ya michezo.
Katika hatua nyingine, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatoa pole kwa klabu ya Simba na wanamichezo wote hapa nchini katika kuomboleza kifo cha kocha Mziray.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Amir Mhando ilieleza kwa wameshtushwa na taarifa za kifo hicho, hivyo wanatoa pole kwa familia ya kocha huyo na wanamichezo wengine katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mwanamichezo huyo mahiri.
Mziray atakumbukwa na waandishi wa habari za michezo kutokana na ukaribu wake na alikuwa na ushirikiano wa kutosha pale alipoombwa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment