29 October 2010

CUF yaivaa NEC.

*Duni adai imekuwa ikisaidia CCM kushinda.

Na Yusuph Katimba
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeshusha tuhuma nzito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), taasisi za utafiti pamoja na Usalama wa Taifa kwa kile kilichodai kutumika kukipa
ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tuhuma hizo zilitolewa na mgombea mwenza wa Urais wa CUF, Bw. Juma Duni Haji katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na maelfu ya wanachama wa chama hicho.

Bw. Duni alidai NEC imekuwa ikijaribu kuhakikisha CCM inaendelea kubaki madarakani huku Usalama wa Taifa ukitumika kutekeleza maagizo mbalimbali yanayotolewa.

Alidai pamoja na kutumia mbinu hizo, pia CCM imekuwa ikitumia Taasisi za Utafiti za REDET na Synovate katika kuwaandaa Watanzania kifikra kuwa bado inapendwa na kukubalika tofauti na uhalisia.

Katika mkutano huo, Bw. Duni aliwaonesha wafuasi wa chama hicho kile alichodai baadhi ya nyaraka za serikali pamoja na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumiwa kutoa maelezo kwa wasimamizi wa vituo vya kura.

Alitoa mfano wa mwaka 2005 katika Wilaya ya Namtumbo, Ruvuma ambapo alidai kuwa chama hicho kilishinda lakini kutokana na maelekezo ya NEC pia usimamizi wa karibu wa Usalama wa Taifa, matokeo yake yalibadilishwa na kukipa ushindi CCM.

Bw. Duni alisema, "kuna dalili zote kuwa CCM wameanza kufanya maandalizi kama walivyofanya mwaka 2005, mwaka huo walisambaza Usalama wa CCM (Usalama wa Taifa) ili kuhakikisha kuwa wanashinda, wakavuruga uchaguzi kwa kusudi na wakajipa ushindi, sasa wanajiandaa tena," alisema.

Akitolea mfano katika Wilaya ya Namtumbo alisema, mtendaji mmoja aliwapa nakala pamoja na vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na tochi, mihuri ya NEC, kura zilizopigwa pamoja na mbinu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa CCM inashinda.

Alisema, mtendaji huyo akiwa na wenzake walipewa maagizo kutoka NEC kuhakikisha kuwa chama hicho kinashinda na kutakiwa kutunza siri na kuongeza kuwa, atakayebainika kutoa siri atafukuzwa.

Barua iliyoandikwa maneno hayo Bw. Duni aliisoma hadharani huku akionesha vifaa vyote ili kuwahakikishia wananchi mikakati ya kuiba kura na kuipa ushindi CCM.

Pia alidai katika kuhakikisha ajenda hiyo inakamilika, Mkuu wa Polisi wilaya hiyo aliletewa ujumbe kutoka NEC kuhakikisha kuwa wafuasi wote wa CUF wanakamatwa ikiwa ni pamoja na kukamata mgombea ubunge wa CUF pamoja na gari lake, (aliionesha barua hiyo).

Alidai CCM katika mikoa na wilaya zote hutumia mbinu hizo ambapo watendaji, wajumbe pamoja na halmashauri za wilaya hutumika katika kuhakikisha kuwa chama hicho kinabebwa.

Katika suala ya REDET na Synovate Bw. Duni alidai kushangazwa kwake na matokeo yao na kwamba mwaka 2005 REDET ilitangaza umaarufu wa Rais Jakaya Kikwete kuwa ni asilimia 80. Baada ya hapo, mwaka 2006 walisema kuwa alishuka na kupata asilimia 63, 2007 alishuka hadi kufikia 57 pia mwaka 2008 alishuka chini ya asilimia 50 ambapo walishindwa kutangaza matokeo hayo.

Alihoji kuwa ni kitu gani alichokifanya Rais Kikwete kwa mwaka 2008/08 na hata kupata asilimia 71 na kudai kuwa hizo ni hila za chama hicho.

"Ninachokumbuka kwa mwaka 2008/09 Rais Kikwete kikubwa alichokifanya ni kwenda kumshika mkono Rais wa Marekani Obama (Barack), labda ndio umaarufu wake umeongezeka kwa hilo," alisema Bw, Duni.

Alisema anashangazwa pia na taasisi nyingine iliyofanya utafiti na kumpa asilimia 38 Rais Kikwete lakini Katibu Mkuu wa CCM Bw. Yusuf Makamba kulalamika na kudai kuwa matokeo hayo hayana ukweli.

Alisema kuwa, kauli ya Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Bara Bw. Pius Msekwa kuwa 'hatujali mashindano ya sera jukwaani' pia kauli yao ya 'ushindi ni lazima' husukuma na kulazimisha ushindi hata kama watashindwa.

Alielezwa kushangazwa kwake na Rais Kikwete kutothamini mchango wa Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bank-Moon huwa anamwomba kumsaidia kazi zake.

Katika mkutano huo Prof. Lipumba alilishukuru Jeshi la Polisi kuwa limewatendea haki. "Jeshi la Polisi kwa upande wetu wametutendea haki, namshukuru sana IGP Said Mwema tofauti na laanakum aliyepita, simtaji jina."

No comments:

Post a Comment