26 October 2010

TFF yaunda Kamati ya Ligi

*Yamzungumzia Asamoah wa Yanga

Na Elizabeth Mayemba
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeboresha kanuni kwa msimu ujao wa ligi, ambapo imeongeza Kamati mpya ya Ligi itakayokuwa inafanya kazi za Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa
TFF, Leodeger Tenga alisema wataunda kamati hiyo ya ligi, ili kuipunguzia mzigo Kamati ya Mashindano.

"Kamati hiyo itaundwa na baadhi ya watu wanaotokea katika klabu, lengo ni kuipunguzia kazi Kamati ya Mashindano," alisema Tenga.

Mbali ya kamati hiyo, Tenga alisema msimu ujao kila klabu ya Ligi Kuu, kabla ya kuanza kwa mashindano inatakiwa kuhakikisha inafanyia mahesabu yake ya msimu uliopita, kwa sababu tayari kila klabu inawatunza fedha wake wa kuajiriwa.

Tenga alisema, pia kila klabu itatakiwa kuwa na uwanja wake wa kufanyia mazoezi, ili zifanye maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kwa mashindano.

Katika hatua nyingine, Tenga alisema suala la mchezaji wa Yanga Kenneth Asamoah, kuichezea timu hiyo msimu huu limeyayuka na kuutaka uongozi wa klabu yake kujipanga kwa usajili wa dirisha dogo.

Wakati huo huo, Tenga ametoa pole kwa ndugu na jamaa wa mashabiki saba wa soka waliofariki katika msongamano, wakati wakijaribu kuingia uwanjani kushuhudia mechi, kati ya timu kongwe nchini humo, Gori Mahiya na AFC Leopard.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Tenga alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo, na kuwapa pole ndugu, marafiki na mshabiki wote wa Kenya kwa kupatwa na msiba huo uliotokea Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Nyayo.

No comments:

Post a Comment