26 October 2010

Shibuda aachiwa huru

*Ajifananaisha na Nyerere

Tumaini Makene na Suleiman Abeid
MGOMBEA ubunge Jimbo la Msawa Magharibi kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Shibuda ameachiwa na polisi, huku akitamba kuwa kukamatwa kwake ni hila sawa na zile alizofanyiwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alipotiwa kifungoni na wakoloni wakati akipigania uhuru.

Amesema kuwa kukamatwa kwake kunadhihirisha namna Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyotumia taarifa potofu kuhukumu watu.

Bw. Shibuda ambaye taarifa zilizolifikia Majira na kuthibitishwa na yeye mwenyewe zinasema kuwa aliachiwa jana jioni, alisema kuwa kukamatwa kwake kunazidi kuifedhehesha CCM mbele ya watu makini, kudhihirisha kuwa kimeacha misingi ya katiba yake iliyotetea wanyonge, kupinga uongo na kutetea ukweli.

Mgombea huyo ambaye kabla ya kuhamia CHADEMA katikati ya mwaka huu, alikuwa mmoja wa makada kindakindaki wa CCM, alikamatwa Ijumaa iliyopita baada ya tukio la wanachama wa vyama viwili vya CHADEMA na CCM, kupigana na kisha mmoja kufariki katika mapigano hayo, mwishoni mwa wiki iliyopita.

"Kwanza niseme tu kuwa nimesikitishwa sana na kifo cha kijana yule, Steven Kwilasa ambaye pia ni mjukuu wangu, maana si kwamba amekufa akipigania itikadi za CCM wala CHADEMA...lakini nashukuru pia kuwa kauli yangu niliyoitoa pale mkutanoni ilisaidia kuepusha vurugu zaidi na pengine mauaji zaidi, maana mimi sikuwa na habari nikashtuka kuona watu wanazidi kupungua mkutanoni, nikauliza kulikoni.

"Nikajibiwa kuwa kuna vurugu zinaendelea, nikawaambia baadhi yao waende kutuliza vurugu hizo na kuhakikisha wanawakamata wanaohusika kwani tayari nilishapiga simu polisi ili watakapokuja waje wawachukue watuhumiwa pale mkutanoni, ndicho kilichofanyika, lakini nikashangaa kuona baada ya mkutano nami nikakamatwa bila kujua sababu.

"Nilivyofikishwa kituoni ndiyo nikaambiwa kuwa nimekamatwa kwa sababu nahusika na mauaji ya mtu ambaye wakati huo nilikuwa sijamjua hata kama ni ndugu yangu, lakini leo nimeachiwa hakuna shutuma yoyote wala hakuna ukweli wowote, najipanga kuendelea na kampeni zangu," alisema Bw. Shibuda.

Bw. Shibuda pia alieleza kusikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari na viongozi wa CCM kuamua kumhusisha yeye na chama chake cha CHADEMA katika mauaji hayo bila kuwa na ushahidi wowote, hususani ule wa upande wa pili ili kujiridhisha na kile kilichotokea kabla ya kuzungumza au kuripoti habari hizo.

Alisema kuwa mpaka jana alikuwa amefanya juhudi kubwa kuwazuia wananchi wa Maswa, wakiwemo wengine kutoka katika Kijiji cha ambako tukio la kuuawa kwa Bw. Kwilasa lilitokea, wasiandamane, katika kuonesha kuwa wanautambua uhalisia wa kile kilichotokea, wakipinga yeye kuhusishwa na mauaji hayo moja kwa moja.

"Kwa kweli kukamatwa kwangu kumezidi kudhihirisha kuwa Serikali ya CCM imekuwa ikitumia taarifa potofu kuhukumu watu...nasikitishwa na mtu kama Makamba (Yusuf) Katibu Mkuu mzima wa chama kama CCM kuamua kutumia taarifa za upande mmoja kuzungumza katika mkutano wa hadhara, kunihusisha mimi na CHADEMA kwenye tukio hili bila hata ya kutaka kupata upande wa pili unasemaje.

"Amefika hapa hakutaka hata kuja kuniona, anatumia taarifa za upande mmoja...unajua ukiwa namna hiyo halafu baadaye unakuja kupata taarifa kamili na sahihi unaonekana wewe ni mtu mzima ovyo, viongozi wa namna hii ndiyo wanamdhalilisha Kikwete...CCM kimeacha misingi yake ya kutetea wanyonge, kinazidi kujifedhehesha kwa sababu wananchi wanaujua ukweli," alisema na kuongeza;

"Akasababisha hata gazeti la (analitaja) likaandika habari ya uongo, juu ya tukio hilo...maana yake ni kwamba CCM kinatumia taarifa za uongo kuhukumu watu...waandishi wengine nao wakaamua kuniita mimi muuaji bila hata kutafuta ukweli upande wa pili hata kwenda tu pale kijijini lilikotokea tukio... lakini nawashukuru Watanzania wote na waandishi wa habari walioutafuta ukweli kwa kuja Maswa."

Alisema pia kuwa kuna dalili mbaya inaanza kujitokeza kuwa tamko lolote kutoka kwa viongozi wa CCM linaonekana kana kwamba limetolewa na serikali kisha linachukuliwa uzito mkubwa na vyombo vya serikali na kufanyiwa kazi, akisema hali hiyo si sahihi.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewataka wafuasi wa vyama vya CCM na CHADEMA wilayani Maswa kuwa watulivu wakati tume maalumu ya kitaifa iliyoundwa ikifanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini chanzo cha vurugu zilizotokea katika kampeni wilayani Maswa na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Daudi Siasi, Tume hiyo inaongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Bw. Robert Manumba tayari ilianza kazi hiyo ya uchunguzi kuanzia juzi.

Kamanda Siasi alisema uchunguzi unaofanyika umelenga kubaini chanzo cha vurugu hizo na kuona iwapo Bw. Shibuda alihusika katika kuandaa vurugu hizo.

Hatua hiyo ya kuundwa kwa tume hiyo inafuatia vurugu kubwa zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko wilayani Maswa katika kijiji cha Kizungu ambapo wafuasi wa CCM na wale wa CHADEMA walishambuliana na kusababisha kifo cha Bw. Kwilasa.

No comments:

Post a Comment