Na Ali Suleiman, Zanzibar
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaye ni mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuheshimu matokeo ya
uchaguzi na endapo atashindwa atampongeza aliyeshinda.
Bw. Hamad alisema hayo wakati aliporudisha fomu za kuwania nafasi hiyo na kuweka wazi kuwa ana matumaini makubwa kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Maalim alisema kwamba atakubali matokeo ya aina yoyote katika uchaguzi huo, kama kushindwa au kushinda kwani huo ndiyo uchaguzi.
Kauli hiyo ya Maalim Seif inaashiria matumaini mapya ya kuwapo kwa amani na utulivu Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Kauli hiyo inakumbusha mambo yaliyotokea Zanzibar katika chaguzi tatu zilizopita, ambapo kiongozi huyo alikataa matokeo, akidai kwamba ameporwa ushindi wake, hali ambayo imekuwa ikisababisha vurugu na mwaka 2001 ilisababisha watu zaidi ya 20 kuuawa na polisi Kisiwani Pemba na wengine mamia kukimbilia nchini Kenya kama wakimbizi.
Tofauti na miaka ya nyuma, safari hii Maalim Seif alikiri kuwapo dalili za uchaguzi mkuu kuwa huru na haki baada ya kuridhishwa na kura ya maoni ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
"Mimi natumai kwamba Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa huru na haki. Tumeona kura ya maoni zoezi lake lisimamiwa vizuri na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)," alisema.
Maalim Seif aliitaka ZEC kuhakikisha kwamba inatoa matokeo ya kura za urais mapema kwa kuwa kazi hiyo itakuwa imerahisishwa kwa kiasi kikubwa katika vituo wilayani.
Alisema hakuna sababu ya kuchelewa kutoa matokeo ya kura za urais kwani mazingira na jiografia ya Zanzibar ni ndogo tofauti na Tanzania Bara.
"Kitendo cha kuchelewa kutoa matokeo ya kura za urais wa Zanzibar ndiyo chanzo cha matatizo. Hakuna sababu ya kuchelewesha matokeo ya urais," alisema Seif.
Alisema mara baada ya uchaguzi mkuu matumaini yake ni kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo itazika kabisa chuki na tofauti za kisiasa kwa wananchi wa Zanzibar.
Serikali hiyo itaundwa kutokana na mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ambayo ilipitishwa na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Maalim Seif alitoa kilio chake cha muda mrefu cha kupingwa kwa wafuasi wake wengi katika daftari la kudumu la wapiga kura na hivyo wanachama hao kutopiga kura uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
"Hicho ndiyo kilio chetu kikubwa...sekretarieti ya tume ya uchaguzi imewapiga panga wafuasi wetu wengi ambao hakuwaorodheshwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na hawatopiga kura uchaguzi mkuu," alisema Seif na kuongeza kwamba kasoro hizo zinatakiwa kuondoshwa mara moja.
Maalim Seif alikabidhi fomu za kusaka wadhamini wapatao 200 kwa mkurugenzi wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar, Bw. Salum Kassim zikiwa zimekamilika baada ya kufanyiwa ukaguzi wa awali.
"Nimepokea fomu za wadhamini kwa ajili ya kuomba nafasi ya urais wa Zanzibar. Tunazifanyia kazi zaidi kwa ajili ya kuzihakiki kuona kwamba zinakidhi mahitaji na masharti kwa mujibu wa katiba," alisema Bw. Kassim.
Wanachama na wafuasi wa chama cha CUF walihudhuria kwa wingi urejeshaji fomu ya kuwania urais wa Zanzibar ambapo msururu mkubwa wa magari yaliwabeba wafuasi hao ukiingia katika ofisi za Tume ya uchaguzi ziliopo Maisara.
Maalim Seif anakuwa mgombea wa kwanza wa nafasi ya urais wa Zanzibar kurudisha fomu za urais. Aliwahi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa kwanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 wakati huo akipambana na Dkt. Salmin Amour ambapo aligombea tena na kuchuana na rais Amani Abeid Karume katika mwaka 2000 na sasa anapambana na mgombea mwengine wa CCM ambaye ni Dokta Ali Mohamed Shein.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment