* Yaiengua Yanga kileleni
Na Theonista Juma, Bukoba
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jana iliiondoa kileleni Yanga na kushika usukani wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1 katika mechi ya
ligi hiyo, iliyochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa matokeo hayo Simba sasa imefikisha pointi pointi 24 na kuiacha Yanga iliyokuwa ikiongoza kwa tofauti ya mabao kwa kuwa na pointi 22 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa Simba iliandika bao la kwanza dakika ya 24 na Rashid Gumbo kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Tonny Ndolo kuunawa mpira eneo la hatari.
Baada ya kufungwa bao hilo, Kagera walikuja juu kutaka kusawazisha bao hilo ambapo Gaudence Mwaikimba alishindwa kufunga bao la wazi dakika ya 30 baada ya kupata nafasi ya kuuweka mpira kimiani.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini hata hivyo Simba ndiyo iliyofanikiwa kuongeza bao la pili dakika 65 kupitia kwa Gumbo, ambaye alikutana na mpira uliotemwa na kipa wa Kagera ambaye alishindwa kuzuia shuti la Emmanuel Okwi.
Baada ya kufungwa bao hilo mpira ulilazimika kusimama kwa dakika 10, kutokana na wachezaji wa Kagera kugomea bao hilo kwa madai kuwa kabla ya kufungwa bao mpira ulikuwa umetoka nje.
Naye Nickson Mkilanya anaripoti kutoka Morogoro kuwa, Yanga jana ilibanwa mbavu na African Lyon kwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri na hivyo kuiacha Simba ikielea kileleni.
Katika mechi hiyo, Yanga ndiyo ilioanza kupata bao dakika ya 78, kupitia kwa Jeryson Tegete kwa shuti kali akiunganisha krosi ya Athuman Idd 'Chuji'.
Baada ya kufungwa bao hilo, African Lyon ilikuja juu kwa kuliandama lango la Yanga na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 88 kupitia kwa Idrisa Rashid kwa mpira wa adhabu uliojaa wavuni moja kwa moja.
Katika mechi hiyo Yanga, itabidi kujilaumu baada ya washambuliaji wake walioongozwa na Tegete kukosa mabao ya wazi.
Nayo Azam FC jana iliondoka kifua mbele katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma baada ya kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0, kupitia kwa Peter Senyonjo dakika ya 10.
Katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Toto African ilishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kutoka suluhu na Majimaji.
Nayo Mtibwa Sugar jana iliondoka kifua mbele baada ya kuifunga AFC mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Manungu.
Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Said Bahanuzi dakika ya 23, Ally Ally dakika ya 26 na Juma Jafari dakika ya 45.
No comments:
Post a Comment