KABUL,Afghanistan
BAADA ya kukaa kimya kwa muda mrefu,kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Bw. Osama bin Laden ameibuka tena safari akiionya Ufaransa kuhusu hatua yake ya kupiga marufuku kuvaa hijabu katika maeneo ya umma ni kuvuruga haki ya raia wake na kuwafanya wapiganaji wake kuendelea kuwashikilia mateka saba wakiwemo raia watano wa Ufaransa.
Bw.Bin Laden alitoa onyo hilo juzi kupitia mkanda wa video uliooneshwa na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera ambapo alisema kuwa mateka hao waliotekwa mwezi uliopita na kikundi cha mtandao unaojiita jihadiast chenye tawi lake katika Jangwa la Sahara lililopo Kaskazini mwa Niger kuwa hilo ni onyo dhidi ya nchi hiyo.
Mbali na onyo hilo kupitia mkanda huo wa video,kiongozi huyo aliitaka Ufaransa kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan.
“Umekwenda kinyume kwa kuamua kwamba una haki ya kuwapiga marufuku wanawake wa Kiislamu kuvaa hijabu,itakuwa siyo haki yetu kulipiza kisasi kwa hatua yako kwa kuwaua mateka raia wako?”alihoji Bin Laden. “Utekaji wa wataalamu wako nchini Niger unahusiana na dhuluma uliyoifanya dhidi ya taifa la Waislamu,"aliongeza.
"Inawezekana vipi kuingilia masuala ya Waislamu, hasa katika maeneo ya Kaskazini na Magharibi mwa Afrika, na kusaidia mawakala wako dhidi yetu na kutumia sehemu kubwa ya rasilimali zetu kupitia ushirikiano na watuhumiwa wakati watu wetu wanakabiliwa na umaskini na tabu, "alisema katika hotuba hiyo ambayo ilidumu kwa dakika 1 na sekunde 55
Mateka hao saba watano wakiwa ni raia wa Ufaransa na wawili ni raia `wa Togo na Madagascar walitekwa usiku wa kati ya Septemba 15 na Septemba 16 katika mji wenye utajiri wa madini ya Uranium nchini Niger.
Vyombo vya usalama nchini humo vinaamini kuwa huenda mateka hao wanashikiliwa katika Jangwa la Sahara upande wa nchi jirani ya Mali.
Katika mkanda huo,kiongozi huyo wa Al-Qaeda aliionya serikali ya Ufaransa kuwa muendelezo wa majukumu yake katika kikosi cha NATO kilichopo nchini Afghanistan itakuwa ni kuhatarisha hali ya usalama nchini kwake.
“Ili kulinda usalama wa nchi yako ni kuondoa dhuluma dhidi ya taifa letu na jambo moja la muhimu ni kujiondoa katika mkondo wa vita wa Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush nchini Afghanistan,”ulisema ujumbe huo ambao ulikuwa na sauti ambayo kwa haraka haikuweza kutambulika
“Ni kwa vipi unaweza kushiriki kuchukua nchi yetu na kuwasaidia Marekani kuua watoto wetu na wanawake na kisha ukatarajia kuishi kwa amani na salama?” ulihoji ujumbe huo.(AFP)
No comments:
Post a Comment