29 October 2010

CHADEMA yasimamishwa kampeni Maswa.

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesimamishwa kuendelea na kampeni katika Jimbo la Maswa Magharibi kutokana na vurugu zilizotokea baina yake na
Chama Cha Mapinduzi  zilizosababisha mtu mmoja kuuawa hivi karibuni.

Taarifa za kusimamishwa zilitolewa jana na Meneja wa kampeni wa Chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana huku akionesha kusikitishwa na hatua hiyo iliyowaathiri wagombea wote wa udiwani, ubunge na urais.

“Huo ni uonevu dhahiri, kwa sababu suala la Maswa bado liko chini ya uchunguzi wa polisi, pia mgombea wetu Shibuda (John) alikamatwa na akaachiwa huru baada ya kuonekana hana kosa wala hakuhusika na tukio la mauaji, lakini haingii akilini unafungia kampeni za chama chote.

“Pamoja na kuwa tumefungiwa wananchi wanapaswa kujua kuwa hatujaondolewa kwenye uchaguzi, na Mabere Marando yuko njiani sasa kwenda Maswa kuwafikishia ujumbe sahihi wananchi, hao bado ni wagombea halali,” alihoji Prof. Baregu.

Huku akisema kuwa kampeni za wagombea wao katika ngazi mbalimbali zinaendelea vizuri, aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kuwapigia kura kama walivyofanya wakati wa mikusanyiko ya mikutano ya kampeni.

Aliongeza kuwa chama chao kimejipanga kulinda kura za wagombea wake, hususan kwa kuweka mawakala waaminifu, wenye uchungu na nchi yao, walio tayari kufanya kazi bila hata ya malipo ya aina yoyote.

Profesa Baregu pia alizungumzia ukimya wa CCM juu ya vijana wa ulinzi, Green Guards, ambao wanadaiwa kuwekwa kambini na kupatiwa mafunzo ya ukakamavu wa kijeshi katika maeneo mbalimbali nchini,  kuwa unatia wasiwasi kuwa wanaandaliwa kufanya jambo, hasa uvurugaji wa amani, wakiwa na lengo maalumu ili baadaye wahusishwe watu wa vyama vingine kuwa ndiyo wanahusika na vitendo hivyo.

“Nafikiri jana mmesikia press conference (mkutano na vyombo vya habari) ya Kinana (Abdulrahman, Meneja Kampeni CCM), amezungumzia juu ya yale yaliyotokea juzi Mwembe Yanga, akisema ni matusi…inawezekana kweli labda mgombea wetu kijana yule alishindwa kulinda lugha yake, maana lugha ya matusi inaweza kuwa na tafsiri tofauti…

“Lakini Kinana anataka kuonesha kuwa CHADEMA kama chama ndiyo kinahusika, hata malalamiko yake NEC ameyawasilisha hivyo, hiyo inatusikitisha sana, maana anajua kuwa hata katika makubaliano yetu ya vyama na NEC, kuna makosa mengine ni ya vyama na mengine ni ya wagombea wenyewe, si kila tendo atakalofanya mgombea utalihusisha na chama…lakini tunashindwa kuelewa, kwanini CCM wanakuwa wepesi kuzungumzia haya, wakati mengine hawataki,” alisema Prof. Baregu na kuongeza;

“Kwa mfano hawataki kabisa kuzungumzia suala la green guards (vijana wa CCM wa ulinzi), hata jana nilikuwa na mtu wao mmoja anaitwa Mkama…Willison Mkama katika kipindi cha televisheni, nikamwambia azungumzie juu ya vijana hao akashindwa. Kuna jambo linafichwa hapa…vijana hao wanapewa mafunzo ya kijeshi, wanaandaliwa kuja kufanya vurugu wakiwa na lengo maalumu wakitaka kuonesha kuwa waliofanya hivyo ni wapinzani, alisema Prof. Baregu.

Prof. Baregu pia alizungumzia kile alichodai ni ‘uchafu’ wa daftari la kudumu la wapiga kura, akisema kuwa wamegundua makosa kadhaa katika daftari hilo, wakitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inatoa mwongozo sahihi juu ya mapungufu yanayoendelea kujitokeza.

Alisema baada ya CHADEMA kupata daftari hilo katika nakala ya kielectroniki kwa msaada wa NEC, mpaka jana wataalamu wao wa  masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) walikuwa wamegundua makosa kadhaa kama vile watu kuandikishwa mara mbili, picha ya mtu mmoja kuonekana ikiwa na majina mawili tofauti, huku waandikishwaji wengine wakiwa wana umri chini ya ule unaoruhusiwa wa miaka 18.

No comments:

Post a Comment